Kansela Merz afanya ziara nchini India
13 Januari 2026
Kansela Friedrich Merz, ameonesha wasiwasi kuhusu namna ushawishi wa kisiasa unavyoziandama benki kuu za ulimwengu. Kiongozi huyo wa Ujerumani amezungumzia wasiwasi huo akiwa katika ziara yake nchini India.
Kansela Merz hivi leo akiwa mjini Bengalore katika siku ya pili ya ziara yake nchini India yenye lengo la kuimarisha uhusiano wa kibiashara, ametilia mkazo juu ya haja ya kuweko uhuru kwa benki kuu za mataifa ya ulimwengu kuachwa kujiamulia bila ya kuingiliwa kisiasa.
Akitaja mfano wa namna Umoja wa Ulaya, ambako Ujerumani ni sehemu, kwa miaka zilivyohakikisha uhuru wa benki kuu ya kanda hiyo unavyozingatiwa,akisisitiza kwamba anatarajia hali itakabakia kuwa hivyo barani Ulaya.
Merz amesema amekuwa na wasiwasi kwa kipindi cha hivi karibuni kuhusu ushawishi wa kisiasa unavyozidi kutumika kuziendesha benki kuu duniani.
Jana Jumatatu akiwa kwenye mji wa Ahmedabad kiongozi huyo wa Ujerumani alidokeza uwezekano wa kusainiwa mkataba wa kihistoria wa biashara huria kati ya Umoja wa Ulaya na India, kufikia mwishoni mwa mwezi huu wa Januari. India
Hatua ambayo huenda ikabadilisha mwelekeo wa mahusiano ya kibiashara duniani kukiweko kiwingu cha kuongezeka mtindo wa kila nchi kuzuia ushindani wa kibiashara huku mazungumzo kati ya India na Marekani yakiwa bado yamekwama.
"Hususan kwa kuzitazama hivi sasa siasa za kimaeneo na mabadiliko ya ghafla ulimwenguni,tunamtazamo sawa wa kimaslahi katika kuimarisha uhusiano wetu wa kimkakati. Kama ilivyo muhimu kwa mahusiano ya Ulaya na mataifa ya Trans Atlantiki yalivyo kwetu Ujerumani, tunapaswa hivi sasa kutanuwa zaidi mtandao mkubwa wa ushirikiano na tunahitaji kufanya hivyo haraka kubakia kuwa na nguvu. India ni mshirika Ujerumani iliyemchagua linapohusika hilo.''
Baada ya kukutana na waziri mkuu Narendra Modi jana katika mji wa Ahmedabad aliwaambia waandishi habari kwamba viongozi wa ngazi za juu wa Umoja wa Ulaya watakwenda India kusaini makubaliano ya biashara huria mwishoni mwa Januari ikiwa mazungumzo yatakamilika kwa kipindi kilichowekwa.
Makubaliano hayo ya kibiashara yanayojadiliwa kwa miaka, yanatajwa kama fursa kwa pande zote mbili ya kuimarisha mahusiano ya kiuchumi na kuumaliza utegemezi wao kwa China na Urusi.Ujerumani na India zakubaliana kuimarisha usalama na uchumi
Kiwango cha biashara kati ya India na nchi za Umoja wa Ulaya ilifikia jumla ya Yuro bilioni 120 mnamo mwaka 2024 na kuifanya jumuiya hiyo ya Umoja wa Ulaya kuwa mshirika mkubwa zaidi wa kibiashara wa India.
Mazungumzo yalipata msukumo zaidi tangu Marekani chini ya rais Donald Trump kuongeza ushuru kwa bidhaa za kutoka India huku pia Trump akiitia kishindo New Delhi kuacha kununua mafuta kutoka Urusi.