1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kansela Scholz ahimiza umoja katika salaam za mwaka mpya

31 Desemba 2021

Katika salaam zake za kwanza za mwaka mpya kwa taifa, kansela Olaf Scholzs ametoa wito kwa umma wa Ujerumani kuungana kupambana dhidi ya janga la covid-19, na kuunga mkono mipango ya serikali yake ya kulifufua taifa.

Deutschland Berlin | Neujahrsansprache | Olaf Scholz
Picha: Kay Nietfeld/dpa/picture alliance

Scholz, ambaye alimrithi Angela Merkel kama kansela mwanzoni mwa mwezi Desemba, amewatolea wito Wajerumani wote kupata chanjo, katikati mwa wimbi kubwa la tano la maambukizi nchini humo, yanayochochewa na kirusi cha corona aina ya Omicron.

Kilichomuhimu hivi sasa ni kasi. Tunapaswa kwenda haraka kuliko kirusi chenyewe. Tangu katikati mwa November, tumeweza kutoa chanjo zaidi ya milioni 30 nchini Ujerumani, zaidi ya taifa lolote ndani ya Umoja wa Ulaya," alisema Scholz.

Soma pia: Scholz ayaainisha malengo yake bungeni kama kansela

"Hilo ni jambo zuri, lakini tunataka kufanya hata bora zaidi. Tunataka kufanikisha chanjo nyingine milioni 30 kufukia mwishoni mwa Januari ili tuwe tayari kujilinda dhidi ya Omicron. Tufanye kila kitu pamoja, na namaanisha kweli kila kitu, ili hatimaye tuweze kuvishinda virusi vya corona katika mwaka mpya."

Scholz amewaomba kuwepo na uelewa kuhusu vikwazo vilivyokazwa pakubwa ambavyo vimeanza kutekelezwa nchini Ujerumani, ikiwemo kupunguza idadi ya watu kwenye mikusanyiko binafsi. Kansela huyo amesema aina mpya ya kirusi cha corona inaenea hata kwa urahisi zaidi kuliko aina zilizotangulia.

Kansela Scholz akizungumza na Wajerumani katika hotuba yake ya kwanza ya kuukaribisha mwaka tangu kuchaguliwa katika wadhifa mwanzoni mwa Desemba 2021.Picha: Kay Nietfeld/dpa/picture alliance

Kansela Scholz amewatolewa wito wakosoaji wa hatua za serikali, ambao baadhi yao wamegeukia vurugu katika wiki za karibuni, kuheshimu mitazamo inayotofautiana na ya kwao, akisema wakati wote kutakuwa na tofuati za kimatazamo, "lakini jamii imara inaweza kuhimili utata, iwapo tutasikilizana na kuonyeshana heshima."

Mwanzo mpya

Mbali na kukabiliana na janga la covid-19, changamoto kubwa zaidi ilikuwa kuweka msingi wa maendeleo zaidi ya Ujerumani. Scholz amesema miaka ya 2020 itakuwa muongo wa mwanzo mpya, na kuongeza kuwa serikali yake ya muungano wa kati kushoto inalenga kuubadili uchumi wa Ujerumani.

"Tutafanikiwa kumudu vyema mabadiliko makubwa ya zama zetu kwa pamoja na kama jamii, ikiwa tutabaki pamoja kama jamii", alisema kansela Scholz.

Soma pia: Kansela Olaf Scholz atoa zingatio kwa Ulaya katika ziara yake ya kwanza

Wakati ambapo Ujerumani inaanza zamu yake ya uongozi wa kundi la mataifa saba yaliostawi zaidi kiuchumi duniani, kansela Scholz ameahidi kutumia nafasi hiyo kuendeleza kundi hilo na kuwa linalooongoza katika juhudi zake za kufanikisha ukuaji unaozingatia utunzaji wa mazingira na kujenga ulimwengu wenye usawa wa kijamii.

"Tutatumia urais wetu ili kundi hili liwe liongoze njia. Liongoze njia ya ufanyaji bishara unaozingatia uhifahi wa mazingira na dunia ya haki," alisema Kansela Scholz.

Ziara ya kwanza ya Kansela Olaf Scholz

01:04

This browser does not support the video element.

Katika wadhifa wake uliopita kama naibu kansela na waziri wa fedha, Scholz alipendekeza kwamba Umoja wa Ulaya uungane na mataifa kama vile Marekani, Canada na Japan kuund akile alichokiita "klabu ya tabianchi", ambamo wanachama wanakubaliana juu ya sheria za pamoja na viwango sawa juu ya namna ya kupunguza utoaji wa gesi chafu.

Lengo la klabu kama hiyo litakuwa siyo tu kuharakisha uhamaji wa dunia kuelekea uchumi rafiki kwa tabianchi, bali pia kuepusha misuguano ya kibiashara inayohusishwa na mifumo mbalimbali ya ushuru, kama vile ushuru wa kaboni unaopangwa kutozwa na Umoja wa Ulaya.

Hiyo pia ndiyo sababu kwa nini muungano mpya wa Ujerumani umedhamiria kuimarisha Umoja wa Ulaya, alisema Scholz, ambaye alimrithi kansela wa muda mrefu Angela Merkel mapema mwezi Desemba. Amesema lengo la serikali yake ni Ulaya iliyo imara, ambayo inaishi kulingana na maadili ya watu, utawala wa sheria na demokrasia.

Ahadi kwa Ukraine

Kuhusu suala la Ukraine, ambako mataifa ya magharibi yanatiwa wasiwasi na ulundikaji wa majeshi ya Urusi karibu na mpaka wa taifa hilo, Scholz amekariri kwamba mamlaka ya mipaka ya Ukraine laazima iheshimiwe, na kusema Ujerumani itaendelea kufanya kazi kwa karibu na washirika wa kanda ya Atlantiki kuhakikisha amani.

Soma pia: Scholz ateua Baraza Jipya la Mawaziri Ujerumani

"Tukiwa na mtazamo juu ya Ukraine, kuna changamoto mpya hapa. Suala la kuheshimu mipaka ya Ukraine ni la thamani kubwa kwetu, na halina mjadala," alisisitiza kansela Scholz.

Scholz achukua usukani kutoka kwa Merkel kama kansela wa Ujerumani

01:19

This browser does not support the video element.

Mzozo umeongezeka pakubwa katika wiki za karibuni kuhusiana na taifa la Ukraine ambalo zamani lilikuwa sehemu ya Jamhuri ya Kisovieti, ambapo wanajeshi wapatao 100,000 wa Urusi walilundikwa karibu na mpaka.

Rais wa Urusi Vladmir Putin aliitwa rasi ya Crimea kutoka Kyiv mwaka 2014 na anatuhumiwa kwa kuchochea vita vya kujitenga vya makundi yanayoelemea Urusi mashariki mwa Ukraine.

Urusi ilielezea uwepo wa vikosi vyake kama ulinzi dhidi ya mataifa ya magharibi yanayosogelea mipaka yake, hasa jumuiya ya NATO, ingawa Ukraine haijapatiwa uanachama katika muungano huo wa kijeshi.

Mazungumzo ya simu kati ya rais wa Marekani Joe Biden na Putin yanapangwa kufanyika mapema mwezi huu, kwa lengo ya kutafuta suluhisho la kidiplomasia juu ya mzozo unaoongezeka kuhusiana na Ukraine.

Chanzo: Mashirika

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW