1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kansela Scholz atafanikiwa kuivuta India kuelekea Magharibi?

24 Februari 2023

India haioneshi ishara za kutaka kubadili msimamo wake kuelekea suala la Urusi na imesema haiwezi kutumia mkutano wa G20 ikiwa kama mwenyekiti kuzungumzia vikwazo vipya dhidi ya Moscow

Deutschland Narendra Modi Staatsbesuch Berlin
Picha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz anaanza ziara yake nchini India na lengo kubwa la ziara hiyo ni kutafuta ushirika wa karibu zaidi na nchi hiyo. Serikali ya Ujerumani mjini Berlin kama zilivyokuwa serikali za nchi nyingine za Magharibi zilipata mshtuko katika kura ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa iliyopigwa baada ya uvamizi wa Urusi nchini Ukraine. India ilijizuia kushiriki kura hiyo.

Ziara ya Kansela Olaf Scholz nchini India ni ya siku mbili na   inafanyika katika wakati ambapo uvamizi wa Urusi nchini Ukraine umeshaingia mwaka wake wa pili na ulimwengu unatafuta namna ya kuumaliza mgogoro huo.

India na China ni miongoni mwa nchi muhimu zikiwa kwa pamoja na idadi ya wakaazi takriban bilioni 2.8 ambayo ni zaidi ya thuluthi moja ya idadi jumla ya ulimwengu.Je, Umoja wa Ulaya utamshinikiza Modi kuhusu Ukraine?

Serikali ya India chini ya waziri mkuu Narendra Modi haikuwahi huko nyuma  na wala haitaki kuunga mkono vikwazo dhidi ya Urusi. Kimsingi nchi za Magharibi hazikuwa na matarajio yoyote China ambayo siku zote unapendelea uchokozi na serikali yake ya chama kimoja, lakini nchi hizo kwa upande mwingine zimeshangazwa sana na India, nchi inayofuata demokrasia.

Picha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Msimamo uliooneshwa na India unamaanisha sio tu serikali ya nchi hiyo haiko tayari kumshinikiza rais wa Urusi Vladmir Putin bali pia umeonesha mshirika huyo wa kimkakati wa Ujerumani haungi mkono mtazamo wa Ujerumani katika suala hilo la kimsingi katika sera yake ya nje. Hata hivyo kwa watu kama Amrita Narlikar, ambaye ni rais wa taasisi kuhusu masuala ya kimataifa na kikanda iliyoko Hamburg (GIGA) msimamo huo wa India haushangazi.

Akizungumza na DW mtalaamu huyo amesema mbali na uhusiano mzuri wa kidiplomasia kati ya India na Urusi, India inaitegemea sana Urusi kwa silaha na kwa namna yoyote India haiwezi kuchezea nafasi hiyo na hasa katika wakati kama huu ambapo inakabiliana na hali ngumu kutoka kwa majirani zake.

Kwa maneno mengine mtaalamu huyo anaamini kile ambacho kinaweza kuleta maana ya kimkakati alau kwa muda mfupi kinaweza kusababisha matatizo makubwa kwa India kwa kipindi cha muda mrefu.Viongozi wa G7 waapa kuisaida Ukraine "bila kuchoka"

Na kwa mtazamo huo mpaka sasa hakuna chochote kilichojitokeza kutoka serikali ya New-Delhi kinachoonesha kubadilika kwa msimamo.

Picha: Isha Bhatia/DW

Na juu ya hilo India pia haina dhamira ya kutumia nafasi yake mwaka huu kama mwenyekiti wa kundi la nchi 20 tajiri na zile zinazoinukia kiviwanda za  G20 kuanzisha mijadala juu ya kuiwekea vikwazo vipya Urusi.

Na hilo kimsingi limeshawekwa wazi na maafisa mbalimbali wa India kwa vyombo vya habari. Na kama haitoshi India imeongeza pia uagizaji wa mafuta kutoka Urusi tangu vilipoanza vita huko Ukraine.

Na ziara ya Kansela Scholz nchi India huenda ikawa ni jaribio la kuivuta nchi hiyo alau kwa kiasi fulani kuegemea upande wa nchi za Magharibi.