1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kansela Olaf Scholz awasili Kenya katika ziara yake Afrika

Daniel Gakuba
5 Mei 2023

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz anaendelea na ziara barani Afrika leo Ijumaa, kwa kufanya mazungumzo na Rais wa Kenya William Ruto mjini Nairobi. Kansela Scholz ameunga mkono Afrika kuwakilishwa katika kundi la G20.

Berlin Präsident William Ruto Kenia und Kanzler Scholz
Rais wa Kenya, William Ruto (kushoto), na Kansela wa Ujerumani Olaf ScholzPicha: Political-Moments/IMAGO

Katika ziara yake nchini Kenya Kansela Olaf Scholz anaambatana na viongozi kadhaa wa makampuni ya biashara kutoka Ujerumani.

Mjini Nairobi amepokelewa na Rais wa Kenya William Ruto na mazungumzo ya kisiasa baina ya viongozi hao yatatuama juu ya matumizi ya nishati endelevu, kupanua uhusiano wa kibiashara na utatuzi wa migogoro.

Soma zaidi: Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz aanza ziara barani Afrika

Hapo jana Kansela huyo wa Ujerumani alitembelea makao makuu ya Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa, ambapo alifanya mazungumzo na rais wa kamisheni ya umoja huo, Moussa Faki Mahamat.

Ziara ya Kansela Olaf Scholz barani Afrika ilianzia nchini Ethiopia Alhamisi (04.05.2023)Picha: DW

Aunga mkono Umoja wa Afrika kuwa na kiti katika G20

Katika mazungumzo hayo Olaf Scholz alisema Afrika inapaswa kuwa na dhima kubwa zaidi katika masuala ya kimataifa, na aliahidi kuwa Ujerumani itaunga Mkono matakwa ya Umoja wa Afrika kuwa katika mikutano ya kundi la G20.

''Nimetoa tamko muhimu hapa katika Umoja wa Afrika. Tunataka kuunga mkono Umoja wa Afrika kupata kiti katika kundi la G20, ili uweze kushiriki na kuwa na kauli. Haya yanatokana na heshima kwa bara la Afrika, nchi nyingi za bara hilo, na idadi ya watu wake inayoongezeka.''

Soma zaidi: Kansela wa Ujerumani kuzuru Kenya na Ethiopia

Pendekezo la Umoja wa Afrika kuwa na nafasi katika mikutano ya kundi la nchi zilizoendelea kiviwanda na zinazoinukia kiuchumi, G20 lilitolewa kwa mara ya kwanza na rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa, na mara moja liliungwa mkono na Rais wa Marekani Joe Biden na wa Ufaransa Emmanuel Macron.

Kiwanda cha nishati ya mvuke nchini Kenya ambacho kitatembelewa na Kansela ScholzPicha: Rick Rycroft/AFP

Uhusiano wa kihistoria baina ya Ujerumani na Kenya

Ujerumani ilikuwa nchi ya kwanza kuitambua Kenya kama jamhuri, baada ya kupata uhuru kutoka ukoloni wa Kiingereza.

Wakati huu Berlin inaichukulia Kenya kama mshirika wake muhimu zaidi katika kanda ya Afrika Mashariki, na mfano mwema kwa uongozi wa kidemokrasia katika eneo hilo.

Soma zaidi: Kenya, Ujerumani kuondowa vikwazo vya ushuru

Kesho Jumamosi, Kansela Scholz atakitembelea kiwanda cha kuzalisha nishati ya mvuke karibu na ziwa Naivasha, kikubwa zaidi cha aina hiyo barani Afrika.

Makadirio tofauti yanaonyesha kuwa kati ya asilimia 80 na 90 ya nishati inayotumiwa nchini Kenya inatokana na vyanzo endelevu, nchi hiyo ikiwa nambari tatu duniani katika sekta hiyo.

 

Vyanzo: dpae, rtre