1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kansela Scholz aendelea na ziara Amerika Kusini

30 Januari 2023

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz anafanya ziara ya siku nne kwenye mataifa ya Amerika Kusini. Scholz anazitembelea nchi za Argentina, Chile na Brazil, katika kile kinachotazamwa kama kuimarisha kwa mahusiano

Chile, Santiago De Chile: Bundeskanzler Olaf Scholz
Picha: Kay Nietfeld/dpa

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz katika ziara yake hiyo kwenye mataifa ya Amerika ya Kusini analenga kusisitiza suala la ulinzi wa hali ya hewa likiwa ni lengo kuu la safari yake.

Argentina kwa upande wake inataka kufikia malengo ya hali ya hewa yaliyopitishwa kwenye mkutano wa Paris ambapo kansela Scholz amemwambia rais wa Argentina Alberto Fernandez kwenye mkutano wao kwamba Ujerumani iko tayari kuisaidia Argentina.

Aliongeza kwamba msaada utalenga kuendeleza ushirikiano katika masuala ya nishati za upepo, nguvu ya jua, nguvu ya maji, na nishati safi ya hidrojeni. Ujerumani inataka kushirikiana kwa karibu na Argentina ili kupunguza utegemezi wake kwa China.

soma Pia:Ujerumani yawakumbuka wahanga wa mauaji ya kuangamiza

Mada nyingine iliyozungumziwa ni vita vya Ukraine ambavyo vimesabaisha hali ya kupanda kwa bei za mahitaji ya kila siku kwa waargentina kama ilivyo katika sehemu zingine duniani.

Hata hivyo Rais wa Argentina, Alberto Fernandez amemwambia kansela Scholz kuwa nchi yake Argentina itaendelea kuiunga mkono Ukraine kisiasa, lakini si kijeshi. Amesema eneo la nchi za Amerika ya Kusini haliko tayari kupeleka silaha nchini Ukraine.

Scholz na Boric wazungumzia mzozo Ukraine

Katika mkondo wa pili wa safari yake katika nchi za Amerika Kusini, kansela wa Ujerumani Olaf Scholz aliwasili Santiago, Chile jana Jumapili.

Kushoto: Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz. Kulia: Rais wa Chile Gabriel Boric.Picha: Ivan Alvarado/REUTERS

katika ziara yake alitembelea jumba la makumbusho pamoja na mwenyeji wake Rais wa Chile, Gabriel Boric na baadae walifanya mazungumzo kwenye ikulu.

Mazungumzo ya viongozi hao yaligusia mada mbalimbali, ikiwa pamoja na vita nchini Ukraine, mabadiliko ya hali ya hewa, na maendeleo ya miradi mipya ya nishati mbadala, ambapo Chile inaweza kuwa kinara wa dunia katika uzalishaji wa nishati ya hidrojeni.

Aidha, Scholz na Boric walitia saini mikataba ya ushirikiano katika teknolojia na uvumbuzi, mafunzo ya uchimbaji madini, uchumi, na nishati.

soma Pia:Serikali ya Ujerumani yaidhinisha vifaru vya Leopard kwa Ukraine

Rais wa Chile ameishukuru serikali ya Ujerumani kwa utayari wake wa kuunga mkono juu ya kutafuta ukweli kuhusu wakazi wake walioteswa, kunyanyaswa kingono na kuuawa na kundi la kidini la mhubiri Paul Schäfer baada ya kukimbia kutoka Ujerumani.

Kundi hilo la Colonia Dignidad ilianzishwa mwaka wa 1961 katika maeneo ya m lima Andes ulio takriban kilomita 350 kusini mwa mji mkuu wa Chile, Santiago.

Kansekla wa Ujerumani Olaf Scholz anatarajiwa kumaliza ziara yake ya siku nne nchini Brazil ambako alisafiri jana usiku hadi mjini Rio de Janeiro ambako atakutana na Rais mpya wa Brazil Luiz Inacio Lula da Silva leo Jumatatu.

Scholz ameandmana na ujumbe wa wafanya biashara, mameneja na wawakilishi kadhaa.

 

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW