1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Scholz: Usalama wa Ujerumani ni kipaumbele

Daniel Gakuba
5 Julai 2023

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amesema usalama wa taifa lake umepewa kipaumbele katika bajeti ya 2024, kutokana na kitisho cha vita vya Ukraine. Hayo ameyasema katika kipindi cha maswali na majibu bungeni mjini Berlin.

Bundestag Kanzler Scholz
Kansela Olaf Scholz wa Ujerumani akizungumza bungeni mjini BerlinPicha: Kay Nietfeld/dpa/picture alliance

Katika kipindi hicho cha maswali na majibu bungeni ambacho huandaliwa mara tatu kwa mwaka, Kansela Olaf Scholz amesema bajeti ya mwaka ujao ambayo imepitishwa na baraza la mawaziri inaonyesha wazi kuwa usalama wa Ujerumani ndilo jambo kuu lililotiliwa maanani, likihusisha msaada kwa Ukraine ili iweze kujilinda dhidi ya uvamizi wa Urusi.

''Usalama ni changamoto kubwa, na hilo bila shaka linamaanisha shinikizo katika bajeti nzima. Kama hali ingekuwa tofauti, kuna mengi ambayo yangeshughulikiwa kwa hali nyingine,'' amesema Scholz na kuongeza kuwa serikali anayoiongoza inafanya kila kinachowezekana kuhakikisha usalama wa nchi, ''kwa kulipatia jeshi vifaa na kuimarisha jumuiya ya Nato''.

Soma zaidi: Scholz ataka Ukraine ipewe hakikisho la usalama 

Mkuu huyo wa serikali ya shirikisho la Ujerumani ameyataja masuala mengine yaliyopewa umuhimu katika bajeti ya mwaka ujao, ambayo yanajumuisha kuendeleza teknolojia ya nishati endelevu ili kuiwezesha Ujerumani kuendelea kuongoza katika sekta ya viwanda bila uchafuzi mkubwa wa mazingira, na pia kugharimia huduma za kijamii na mshikamano wa kitaifa.

Ukumbi wa Bunge la Ujerumani, BundestagPicha: Bernd von Jutrczenka/dpa/picture alliance

Umaarufu wa AfD ni wa muda mfupi tu

Kansela Scholz ameshiriki katika kipindi hiki bungeni siku chache baada ya chama cha sera kali za mrengo wa kulia, AfD kushinda uchaguzi katika miji miwili midogo ya mashariki mwa Ujerumani na kwa mara ya kwanza kuwa na viongozi wa umma wa kuchaguliwa.

Akijibu swali juu ya kuongezeka kwa umaarufu wa chama hicho ambacho kinachukuliwa na vyama vingine vya mrengo wa kati kutokuwa cha kidemokrasia, Scholz amesema anao ''uhakika kuwa mafanikio hayo ni ya muda mfupi tu'' , na kwamba ''katika uchaguzi ujao uungwaji mkono wa chama hicho kinachopinga wahamiaji utakuwa umeshuka na kurudi katika viwango vya uchaguzi mkuu uliopita.''

Mashirika ya kijasusi ya Ujerumani yameyaainisha matawi ya vijana ya chama cha AfD kuwa yenye misimamo mikali iliyopitiliza.

Kwa mara ya kwanza chama cha AfD kimeshinda uchaguzi wa kuiongoza miji mashariki mwa UjerumaniPicha: Jan Woitas/dpa/picture alliance

Vyama vya upinzani vyakosoa rekodi ya Scholz katika uchumi na jamii

Vyama vya upinzani, vikiongozwa na kile cha Christian Democratic Unioni vimemshambulia Kansela Scholz, kwa hoja kwamba serikali yake imeshindwa kuitimiza ahadi ya wakati wa kampeni, kwamba ingepunguza bei ya umeme kwa viwanda, na kumshutumu kushindwa kupambana na mfumko wa bei, mdororo wa uchumi na uhamishaji wa mitaji kutoka Ujerumani kwenda nchi za nje.

Soma zaidi: Uchumi wa Ujerumani waingia katika mdororo

Majibu yake yalikuwa kwamba hana muda wa kutosha kukanusha alichokiita, ''madai yasio sahihi'' ya wapinzani, akisema serikali yake imefanya kila kinachowezekana kuhakikisha kuwa nishati ya umeme inaendelea kupatikana kwa bei nafuu.

Vyanzo: afpd,rtrd

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW