1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merz aahidi kuishinikiza Urusi kusitisha vita Ukraine

11 Oktoba 2025

Msemaji wa serikali ya Ujerumani Stefan Kornelius, amesema Kansela wa taifa hilo Friedrich Merz ameapa kuishinikiza zaidi Urusi kuachana na vita nchini Ukraine.

Kansela wa Ujerumani  Friedrich Merz
Kansela wa Ujerumani aahidi kuishinikiza Urusi kuachana na vita vyake Ukraine Picha: Bundesregierung

Kornelius amesema  katika mazungumzo ya njia ya simu kati ya Merz na rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, Ujerumani iliahidi kuendelea kuiunga mkono Kiev na kuimarisha ushirikiano wake wa kiulinzi.

Zelensky ameishukuru Ujerumani kwa kuendelea kuiunga mkono akisema Urusi imetumia droni na makombora kutekeleza shambulizi aliloliita la kigaidi dhidi ya taifa lake lililolenga miundombinu yake ya nishati.

Wakati huo huo Zelensky pia alizungumza kwa njia ya simu na rais wa Marekani Donald Trump leo Jumamosi na kumtaka awezeshe kufikiwa makubaliano ya amani ya Ukraine kama alivyofanya katika eneo la Mashariki ya Kati.

Zelensky amesema kama vita vinaweza kusitishwa katika eneo moja vinaweza pia kusitishwa katika eneo lengine, akimaanisha uhasama kati ya Ukraine na Urusi ulioanza mwaka 2022 baada ya Moscow kumvamia jirani yake Februari 24.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW