Kansela wa Ujerumani atoa wito kwa taifa la Misri
11 Julai 2013Kansela Angela Merkel amesema Katiba ya Misri inatoa muelekeo utakaofuatwa kwa sasa lakini akaongeza kwamba ni muhimu kwa wanasiasa wa vyama vyote kujumuishwa katika mchakato wote wa uundaji wa serikali ya mpito.
Merkel amesema hiyo ndio njia pekee itakayohakikisha demokrasia inatekelezwa nchini Misri.
Uchaguzi wa bunge unatarajiwa kufanyika katika miezi sita ijayo.
Huku Uchaguzi huo ukitarajiwa kutoa sura kamili ya siasa za Misri, utawala wa mpito unania ya kuiondoa Misri katika ghasia hasa baada ya kuondolewa kwa rais aliyechaguliwa kihalali Mohammed Mursi.
Viongozi wa Mpito wakaribisha tamko la Marekani
Wakati huo huo Viongozi wa mpito wamekaribisha tamko la wizara ya mambo ya nchi za nje ya Marekani, kuelezea uongozi wa Mursi haukuwa wa kidemokrasia.
Msemaji wa wiziara hiyo Jen Psaki amesema wametoa tamko hilo baada ya kuangalia watu zaidi ya milioni 22 wakiandamana kutaka kuondolewa kwa Mursi na kusema kwamba demokrasia sio tu kushinda katika uchaguzi.
Naye msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje wa Misri Badr Abdelatty amesema tamko hilo linaonesha kuwa Marekani inatafakari na kuelewa maendeleo ya kisiasa nchini humo.
Kwa jumla Marekani mpaka sasa imekataa kuiita hatua ya jeshi kama mapinduzi kwa kuwa hii inaweza kuilazimisha kusitisha msaada wa kijeshi wa takriban dola bilioni 1.3 kwa nchi hiyo. Marekani sasa inaendelea na mpango wake wa kupeleka ndege za kivita aina ya F-16 nchini Misri.
Ghasia zaigawa Misri mara mbili
Jeshi lilimuondoa rais huyo Madarakani baada ya mamilioni ya raia wanaompinga kuandamana dhidi yake. Hali hii imelifanya taifa hilo la kiarabu kukumbwa na mgawanyiko ambao haujawahi kuonekana katika historia yake.
Ghasia zilizoonekana wiki hii kati ya wafuasi wa Mursi na wapinzani wake zimezidi kuigawanya nchi hiyo.
Hii leo Waziri Mkuu Hazem al-Beblawi, amesema hatazuia chama cha udugu wa kiiislamu kupata nyadhifa katika baraza lake la mawaziri bora tu wawe na ujuzi wa kushikilia nyadhifa hizo, lakini wafuasi wa chama hicho wamekataa mualiko wa kujiunga na serikali hiyo mpya na kuitisha maandamano makubwa hapo kesho kupinga kile wanachokiita mapinduzi dhidi ya rais wao.
Mwandishi:Amina Abubakar/Reuters/AP
Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman