Kansela wa Ujerumani Merz anakabiliwa na ziara ngumu Israel
6 Desemba 2025
Tangu aingie madarakani miezi saba iliyopita, Kansela wa chama cha siasa za wastani za mrengo kulia cha Christian Democratic Union (CDU) Friedrich Merz amekuwa akiendeleza "uhusiano maalum" kati ya Ujerumani na Israel. Kumekuwa na migogoro kadhaa kati ya Berlin na Jerusalem kuhusu vitendo vya Israel katika Ukanda wa Gaza vya kujibu shambulio la kigaidi lililofanywa na Hamas dhidi ya Israeli mnamo Oktoba 7, 2023, ambalo lilisababisha vifo vya zaidi ya watu 1,200.
Kulingana na wizara ya afya ya Gaza, ambayo Umoja wa Mataifa na mashirika mengi ya haki za binadamu wameiona kuwa ya kuaminika, kiasi ya Wapalestina 70,000 wameuawa katika operesheni za kijeshi za Israel tangu Oktoba 2023. Mashirika mengi ya haki za kimataifa na tume ya uchunguzi ya Umoja wa Mataifa yamegundua kuwa vita vya Israel huko Gaza ni mauaji ya halaiki.
Kwa hivyo ziara ya kwanza ya Merz mjini Jerusalem ni kazi ngumu. Baadhi ya mambo yanajikita katika mwendelezo, mengine yanahusu mabadiliko. Hili tayari liko wazi kutokana na kauli zilizotolewa na balozi wa Israeli nchini Ujerumani, Ron Prosor, akijibu maoni yaliyotolewa na kansela.
Wakati Merz, wiki mbili tu baada ya kuingia madarakani, alipoonyesha wasiwasi wake kuhusu vitendo vya Israel huko Gaza mwishoni mwa Mei na kuzungumzia uvunjaji wa sheria za kimataifa za kibinadamu, Prosor alieleza kwa utulivu: "Friedrich Merz anapotoa ukosoaji huu dhidi ya Israel, tunamsikiliza kwa makini sana kwa sababu yeye ni rafiki," mwanadiplomasia huyo aliiambia televisheni ya umma ya Ujerumani ZDF.
Merz 'atafanya juu chini kudumisha urafiki na Israel'
Wiki kumi na moja baadaye, sauti yake imekuwa tofauti kabisa: mwanzoni mwa Agosti, kwa kuzingatia hali ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza, Merz aliamua kuacha kusambaza zana fulani za kijeshi kwa Israel "hadi taarifa zaidi itakapotolewa." Hasa, hii ilihusu silaha ambazo zinaweza pia kutumika katika vita katika Ukanda wa Gaza. Kulingana na kansela, serikali ya Ujerumani isingepeleka silaha kwa mzozo ambao ungesababisha "mamia ya maelfu ya raia kujeruhiwa au kuuwawa."
Ukosoaji wa Prosor kuhusu uamuzi huo ulikuwa mkali kupita kiasi. Hatua ya kansela haikusababisha kuachiliwa kwa mateka wa Israel kutoka Hamas wala kusitisha mapigano, alikiambia kituo cha habari cha Die Welt cha Ujerumani. Kilichokuwa kikijadiliwa ni "kuweka chini silaha na kuondoka kwa wanajeshi wa Israel," kulingana na Prosor, ambaye pia alisema ilikuwa "sherehe kwa Hamas." Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu pia alizungumzia Merz kuwazawadia Hamas.
Ni kufikia Katikati ya Novemba ambapo serikali ya Ujerumani iliondoa vikwazo vya uuzaji wa silaha kuanzia Novemba 24. Msemaji wa serikali Stefan Kornelius alitaja usitishaji mapigano katika Ukanda wa Gaza ulioanza kutekelezwa Oktoba 10 kama sababu ya hili.
Lakini usitishaji mapigano haujakuwa imara, huku kukiwa na mapigano ya mara kwa mara kati ya wapiganaji wa Hamas na wanajeshi wa Israel, pamoja na mashambulizi ya makombora kutoka kwa vikosi vya Israel huko Gaza. Wizara ya afya ya eneo hilo inaripoti kwamba zaidi ya watu 300 wameuawa katika mashambulizi ya makombora ya Israel kote Ukanda wa Gaza tangu usitishaji mapigano uanze, wakiwemo watoto wengi.
Simu za mara kwa mara kati ya Merz na Netanyahu
Siku ya Jumapili, Merz atakuwa mgeni wa Netanyahu tena. Mara nyingi zaidi kuliko watangulizi wake, kansela huyo hutaja mazungumro marefu ya simu anayofanya na waziri mkuu wa Israel katika taarifa zake, iwe ni kuhusu hali ya jumla katika Mashariki ya Kati, mgogoro wa kibinadamu huko Gaza, au vita vya siku 12 kati ya Israel na Iran.
Haya yalijiri huku kukiwa na maswali kuhusu kama Ujerumani itatekeleza majukumu yake ya kimataifa, kama mshiriki wa sheria za Mahakama ya Kimataifa ya Jinai - ICC, kumkamata Netanyahu — ambaye yuko chini ya kibali cha kukamatwa cha ICC tangu Novemba 2024 kwa uhalifu dhidi ya ubinadamu na uhalifu wa kivita — iwapo atatembelea Ujerumani, kama inavyohitajika kulingana na sheria za kimataifa. Merz alisema mnamo Februari 2025 muda mfupi kabla ya kuchukua madaraka kwamba "Pia nimemuahidi kwamba tutapata njia na mbinu za kuitembelea Ujerumani na pia kuweza kuondoka tena bila kukamatwa nchini Ujerumani."
Mbali na mazungumzo ya kisiasa na Netanyahu na Rais wa Israel Isaac Herzog, ziara ya kansela wa Ujerumani kwenye Makumbusho ya Mauaji ya Kimbari ya Yad Vashem hakika itakuwa muhimu. Eneo hilo linaweka hai kumbukumbu ya Wayahudi milioni 6 waliouawa na Ujerumani ya Utawala wa Nazi katika Mauaji ya Kimbari.
Merz akiri ugumu kuhusu dhana ya 'maslahi ya dola'
Baada ya kuwepo mzozo kuhusu uuzaji wa silaha nje ya nchi, Merz alidai kwamba "urafiki" wa Ujerumani na Israel unaweza kuhimili hali ya kutokubaliana kuhusu suala maalum: "Hakuna kilichobadilika katika suala hilo, na hakuna kitakachobadilika," Merz alisema.
Kwa upande mwingine, Kansela wa Ujerumani anakubali kuwa na ugumu kuhusu dhana ya "maslahi ya dola," kwa sababu "haijawahi kuelezwa wazi kuhusu athari zake," kama alivyosema katika mahojiano ya gazeti moja mnamo Oktoba. Dhana hii ilitumiwa na Kansela Angela Merkel (CDU) mnamo 2008, alipokuwa mkuu wa kwanza wa serikali ya kigeni kuhutubia Knesset, bunge la Israel. "Kila serikali ya shirikisho na kila kansela aliyenitangulia alidhamiria kuheshimu jukumu maalum la kihistoria la Ujerumani kwa usalama wa Israel. Jukumu hili la kihistoria la Ujerumani ni sehemu ya maslahi ya ya serikali ya nchi yangu," Merkel alisema.
Merz sasa anasafiri kwenda Jerusalem, miezi saba baada ya kuchaguliwa kwake kuwa Kansela. Watangulizi wake wawili, Olaf Scholz na Angela Merkel, walifanya ziara zao za kwanza kukutana na mkuu wa serikali ya Israel ndani ya miezi mitatu ya kwanza baada ya kuchukua madaraka. Hakuna hata mmoja wao aliyesimama katika vituo vingine katika safari zao. Merz, kwa upande mwingine, anasafiri kwa ndege kwenda Jordan kukutana na mfalme wa Jordan huko Amman kabla ya kuendelea hadi Israel.
Makala hii iliandikwa kwanza katika Kijerumani.