1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kansela wa Ujerumani asaka nishati kwenye nchi za Ghuba

Zainab Aziz Mhariri:Sylvia Mwehozi
24 Septemba 2022

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz yuko nchini Saudi Arabia kwa ziara ya siku mbili kwenye nchi za Ghuba kwa matumaini ya kufikia mikataba mipya ya nishati na mataifa hayo tajiri yanayozalisha mafuta na gesi.

Bundeskanzler Scholz reist in die Golf-Region und trifft Scholz Kronprinz Salman
Picha: Kay Nietfeld/dpa/picture alliance

Kansela Scholz, ambaye ameandamana na ujumbe mkubwa wa wafanyabiashara wa sekta ya viwanda, alipokelewa katika uwanja wa ndege wa Jeddah na gavana wa eneo la Makkah Mwanamfalme Khalid bin Faisal Al Saud.

Kansela wa Ujerumani akipokelewa na Mwanamfalme Khalid bin Faisal Al Saud mjini Jeddah.Picha: Kay Nietfeld/dpa/picture alliance

Scholz, amekutana na kiongozi wa Saudi Arabia mwanamfalme Mohammed bin Salman na baadae leo Jumamosi Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz na ujumbe wake wataelekea Umoja wa Falme za Kiarabu ambako siku ya Jumapili atakutana na Rais wa UAE Sheikh Mohamed bin Zayed Al-Nahyan na Jumapili hiyo hiyo watakwenda Qatar nchi yenye utajiri wa gesi ambako kansela Scholz atafanya mazungumzo na Emir Sheikh Tamim bin Hamad Al-Thani.

Kansela huyo anatumai atafaulu katika kuanzisha ushirikiano mpya utakaowezesha nchi yake kufikia makubaliano mapya ya nishati na mataifa hayo ya Ghuba yenye utajiri wa mafuta na gesi, ili kuziba pengo la nishati kutoka Urusi tangu nchi hiyo ilipoanza uvamizi wake nchini Ukraine.

Emir wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad Al-Thani.Picha: Bernd Elmenthaler/IMAGO

Hata hivyo kansela Scholz anakabiliwa na mtihani wa kusawazisha maswala ya kidiplomasia, kwani atalazimika kuepuka tofauti kubwa na wenyeji wake kuhusu haki za binadamu.

Hadi hivi karibuni, Mwanamfalme Mohammed bin Salman alitengwa na Marekani na nchi za Magharibi kutokana na kuuliwa kwa mwandishi wa Habari Jamal Khashogi wa jarida la Washington Post aliyeukosoa utawala wa kifalme mnamo mwaka 2018.

Serikali ya Ujerumani ililaani vikali mauaji ya mwanahabari huyo na hata kabla ya kansela kuanza ziara yake vyanzo katika serikali yake vilisema Ujerumani haitabadili msimamo wake kuhusiana na hilo.

Kushoto: Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz. Kulia: Kiongozi wa saudi Arabia Mwanamfalme Mohammed bin Salman.Picha: Kay Nietfeld/dpa/picture alliance

Hata hivyo chanzo kimoja kutoka serikalini kimeeleza kwamba Saudi Arabia kama nchi muhimu inayouza mafuta na yenye  nguvu kubwa katika kanda ya mashariki ya kati inamaanisha pana ulazima wa kuwa na uhusiano thabiti na mwana mfalme Mohamed bin Salman.

Chanzo hicho cha serikali kimesema lazima Ujerumani ifanye kazi na Saudi Arabia ikiwa inataka kusuluhisha, kwa mfano, vita vya nchini Yemen au kushughulikia suala la Iran miongoni mwa maswala mengine.

Ujerumani inataka kuupanua ushirikiano katika teknolojia mpya kama hidrojeni ya kijani inayozalishwa kwa kutumia nishati mbadala, ambayo Ujerumani inaweza kuagiza kwa wingi kutoka mataifa ya Ghuba.

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz.Picha: Michael Kappeler/dpa

Vyanzo vya serikali vinasema kansela Scholz anatakiwa kuimarisha ushirikiano wa kisiasa na mataifa yenye nguvu katika kanda ya Mashariki ya kati, yanayovutwa kwa upande mwingine na Urusi na China.

Vyanzo:AFP/DPA

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW