1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz yupo nchini Senegal

Zainab Aziz Mhariri:Yusuf Saumu
23 Mei 2022

Kansela wa Ujerumani Olaf scholz anafanya ziara yake ya kwanza katika nchi tatu za Afrika. Ameanzia nchini Senegal ambako ameahidi msaada kwa nchi za Afrika zilizoathiriwa na uhaba wa chakula kutokana na vita vya Ukraine

Senegal Besuch Kanzler Scholz | Präsident Macky Sall
Picha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz alianza ziara yake katika mataifa matatu barani Afrika hapo jana Jumapili, ziara ambayo inatarajiwa kujumuisha mazungumzo na viongozi wa Afrika kuhusu siasa za kikanda na athari zinazosababishwa na vita vya Ukraine. Kuhusu mzozo wa sasa wa chakula, kansela wa Ujerumani ametahadharisha kwamba nchi nyingi zinaweza kukabiliwa na matatizo katika kulisha watu wake. Amesema Ujerumani itafanya kila iwezalo kukabiliana na hali hii inayosababisha kupanda kwa bei za vyakula. Nchi zilizolemewa na hali hiyo barani Afrika ni pamopja na za eneo la mashariki ni zile zinazokabiliwa na ukame mkubwa za Somalia, Ethiopia na eneo la kaskazini mwa Kenya.

Kushoto: Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz. Kulia: Rais wa Senegal Macky Sall.Picha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Rais wa Senegal Macky Sall ambaye pia ni mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, kuhusu vita vya nchini Ukraine amemwambia kansela wa Ujerumani kwamba japo vita hivyo vinatokea katika bara jingine lakini bara la Afrika pia limeathirika kwa vita hivyo

Amesema ndio kwa sababu bara la Afrika linataka amani na halipendelei kuingizwa kwenye mzozo huu. rais Sall amesema wanafanya kila wawezalo ili kuhakikisha vita vinasitishwa na kwamba mazungumzo yanafanyika. Rais huyo wa Senegal amesema huo ndio msimamo wa bara la Afrika kulingana na maoni ya viongozui wa bara hilo, amesema muhimu kwa bara la Afrika ni kuhakikisha kuwa watu wake wana chakula cha kutosha, wana usalama thabiti na wanapambana na ugaidi.

Baada ya kansela wa Ujerumani Olaf Scholz kufanya mazungumzo na Rais wa Senegal Macky Sall, kuhusu uzalishaji wa gesi katika pwani ya Afrika Magharibi kwa kushirikiana na Senegal na Mauritania rais Macky Sall amesema Senegal iko tayari kusambaza gesi katika nchi za Ulaya zinazokabiliwa na uwezekano wa kusimamishwa usafirishaji wa nishati hiyo kutoka Urusi.

Kushoto: Rais wa Senegal Macky Sall. Kulia kansela wa Ujerumani Olaf Scholz aliye ziarani nchini Senegal.Picha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Scholz pia amesema Ujerumani itashirikiana na Senegal katika swala la uzalishaji wa gesi. Amesema ni jambo la maana kuzingatia ushirikiano kwa sababu uzalishaji wa gesi ni jambom lilozihusisha pande zote. Senegal ina mabilioni ya mita za ujazo za hifadhi ya gesi na inatarajiwa kuwa mzalishaji mkuu wa gesi barani Afrika. Ujerumani inataka kupunguza utegemezi wake mkubwa wa gesi kutoka Urusi baada ya nchi hiyo kuivamia Ukraine. Afisa mmoja wa serikali ya Ujerumani amesema nchi hiyo inaweza kusaidia katika kufanya utafiti ili kupata maeneo yenye gesi nchini Senegal. Kansela Scholz yuko nchini Senegal na kisha atakwenda Afrika Kusini ambapo nchi zote mbili zimealikwa kuhudhuria mkutano wa G-7 nchini Ujerumani mwishoni Juni.

Vyanzo: DPA/AP

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW