1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kardinali wa Vatican achukua likizo ili kujisafisha

29 Juni 2017

Msaidizi mwandamizi wa kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis, Kardinali George Pell amesema atachukua likizo na kurejea Australia ili kujitetea dhidi ya madai ya kuhusika kwake na unyanyasaji wa kingono.

Vatikan Kardinal George Pell
Picha: picture-alliance/dpa/M. Brambatti

Kardinali George Pell ameutangaza uamuzi huo leo mbele ya waandishi habari katika ofisi ya habari ya Vatican, ambapo amekanusha madai dhidi yake na kusema kwamba atarejea Australia ili aweze kulisafisha jina lake.

Kardinali Pell ambaye ni mkuu wa masuala ya fedha ya Vatican amesema hana hatia na amekuwa akimuarifu Papa Francis katika kipindi chote cha mchakato huo mrefu na amekuwa akizungumza naye hivi karibuni.

''Katika miezi ya hivi karibuni mara kwa mara nimekuwa nikimuarifu Papa Francis, Baba Mtakatifu na tulizungumza kuhusu haja ya mimi kuchukua likizo ili kulisafisha jina langu. Hivyo nina furaha kwamba Baba Mtakatifu amenipa ruhusa ya kuchukua likizo na kurejea Australia,'' alisema Pell.

Papa FrancisPicha: Reuters/R. Casilli

Kardinali huyo mwenye umri wa miaka 76, amesema yuko tayari kusimama mahakamani kujibu shutuma dhidi yake na amebainisha kuwa unyanyasaji wa kingono ni kitendo cha kuchukiza kwake.

Taarifa iliyotolewa na Vatican imeeleza kuwa wafanyakazi katika idara ya Kardinali Pell wataendelea na majukumu yao bila ya kiongozi wao kuwepo. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Papa Francis anaheshimu uaminifu alionao Kardinali Pell pamoja na nia yake thabiti ya kujitoa katika kazi yake ya kuifanyia mageuzi idara ya fedha ya Kanisa.

Papa: Naheshimu mfumo wa sheria wa Australia

Aidha, taarifa hiyo imefafanua kuwa Papa Francis pia amesema anauheshimu mfumo wa sheria wa Australia ambao utaamua kuhusu mashtaka hayo. Kesi hii inaelezwa kuwa aibu kubwa kwa Papa Francis, ambaye alichaguliwa mwaka 2013 na aliyetumia mamlaka yake kulisafisha Kanisa Katoliki na kashfa za kingono pamoja na fedha.

Awali polisi nchini Australia katika jimbo la Victoria walitangaza kuwa Kardinali Pell anashutumiwa kwa makosa ya unyanyasaji wa kingono baada ya kuwepo malalamiko kadhaa kuhusiana na makosa yake ya zamani. Kamishna msaidizi wa Victoria, Shane Patton amewaambia waandishi habari kwamba kulikuwa na malalamiko kadhaa, ingawa hakutoa taarifa zaidi kuhusu mashtaka.

Kardinali George Pell akiwa na Papa mstaafu Benedict XVIPicha: AP

Wakili wa wanaume wawili ambao utambulisho wao haujatolewa na waliotoa malalamiko ya kunyanyaswa na Kardinali Pell, amesema wateja wake wanajisikia furaha sana kutokana na hatua iliyochukuliwa na polisi ya kumfungulia mashtaka Pell.

Kardinali Pell anadaiwa kutenda vitendo hivyo katika miaka ya 1970 wakati akiwa padri katika mji wa Ballarat. Baadae alikuwa Askofu Mkuu wa Melbourne na kisha Sydney.

Kardinali Pell amekuwa afisa wa ngazi ya juu kabisa wa Vatican, kushtakiwa katika kashfa ya unyanyasaji wa kingono inayolikumba Kanisa Katoliki. Anatarajiwa kufika mahakamani mjini Melbourne Julai 18 mwaka huu ili kusikiliza kesi dhidi yake.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/ AFP, AP, DPA
Mhariri: Mohammed Khelef