1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiNigeria

Watu wasiopungua 26 wafa katika ajali ya boti, Nigeria

11 Septemba 2023

Watu wasiopunguwa 26 wamefariki na wengine wengi bado hawajulikani waliko baada ya kivuko kuzama kwenye bwawa moja kubwa huko kaskazini na kati mwa Nigeria jana Jumapili.

Wafanyakazi wa uokozi wakiwa wamebea miili ya wahanga wa ajali ya boti huko Wara Kebbi nchini Nigeria iliyotokea Mei 27, 2021. Zaidi ya watu 100 walikuwa hawajulikani walipo.
Wafanyakazi wa uokozi wakiwa wamebeba miili ya wahanga wa ajali ya boti huko Wara Kebbi nchini Nigeria iliyotokea Mei 27, 2021. Zaidi ya watu 100 walikuwa hawajulikani walipo. Picha: AP/picture alliance

Msemaji wa gavana wa jimbo la Niger, Bologi Ibrahim amesema boti hiyo ilizama ikiwa imewabeba zaidi ya watu 100 wakiwemo wanawake na watoto.

Wahanga walikuwa wakisafiri kwa boti hiyo kuelekea kwenye mashamba yao yaliyoko upande wa pili wa bwawa hilo kubwa. Watu 26 waliothibitika kufariki, wengi ni wanawake na watoto na zaidi ya watu 30 wameokolewa wakati operesheni ya uokozi inayoendeshwa na polisi wa kikosi cha wanamaji, kwa ushirikiano na wapiga mbizi ikiwa bado inaendelea.

Mwezi Julai zaidi ya watu 100 walipoteza maisha baada ya boti iliyofurika abiria kuzama kwenye moja ya wilaya zajimbo la Niger. Huo ulikuwa mkasa mbaya zaidi wa ajali za majini kuikumba Nigeria katika miaka ya karibuni.

Kwa mujibu wa maafisa hiyo ni ajali ya pili kubwa kuwahi kutokea kwenye eneo hilo ndani ya kipindi cha miezi mitatu.