Karzai aomba pesa zaidi kuboresha jeshi la taifa
24 Septemba 2008Rais wa Afghanistan, Hamid Karzai,ahutubia baraza kuu la Umoja wa Mataifa jumatano.
Kwa upande mwingine kiongozi huyo ametoa mwito kwa yeyote atakachukua hatamu za uongozi nchini Marekani baada ya uchaguzi mkuu,kuusadia utawala wa Kabul kwa kuupa msaada nyeti wa kuimarisha jeshi lake.
Rais Karzai kwa sasa yuko New York Marekani kuhudhuria kikao cha baraza kuu la Umoja wa Mataifa.Mapema wiki hii baraza la Usalama la Umoja wa huo, kwa kauli moja, lilirefusha mda zaidi wa vikosi vya kigeni vilivyoko Afghanistan chini ya uongozi wa shirika la kujihami la NATO kubaki huko.
Hata hivyo baraza hilo limekosoa hali ya raia wa kawaida wa Afghanistan kuendelea kuuawa na hivyo kusihi jeshi lake pamoja na vikosi vya Marekani kufanya kila juhudi kupunguza vifo vya raia wa kawaida.
Bw Karzai alipoulizwa hali ya kuongezeka kwa kuuliwa kwa raia pamoja na umaarufu wa kampeini ya kijeshi dhidi ya ukereketwa inayoongozwa na Marekani,rais huyo amesema kuwa nchi yake itakuwa dola maskani,lisilo na muelekeo bila ya msaada wa Marekani na washirika wake.
Aidha alipokuwa katika mkutano ya jamii ya Asia mjini New York alimhimiza yeyote atakaechaguliwa kuiongoza Marekani, afikirie kuiongezea msaada nchi yake, sio tu wa pesa lakini pia msaada wa zana za kijeshi mkiwemo ndege ili kulipiga jeki jeshi lake.
Kwa mda huohuo amegusia hali ya kisiasa katika nchi jirani ya Pakistan.
Amenukuliwa kusema kuwa mabadiliko ya uongozi yaliyotokea nchini Pakistan hivi majuzi,kwa mara ya kwanza, yametoa matumaini ya kupatikana kwa ushindi katika vita dhidi ya ugaidi na hivyo kuomba kufanyika hujuma zaidi za pamoja dhidi ya maficho ya wakereketwa yaliyoko katika mpaka wa Pakistan na Afghanistan.
Vilevile ameiomba Marekani kuunga mkono utawala mpya wa rais Asif Ali Zardari,kuupiga vita ukereketwa.Zardari alichukua utawala wa nchi hiyo kutoka kwa Generali Pervez Musharraf.
Uhusiano kati ya nchi hizo jirani haukuwa mzuri wakati wa utawala wa Musharraf.Kiongozi wa Afghanistan amekuwa kila mara akiunyoshea kidole utawala wa Islamabad wa kutofanya la kutosha ili kukabiliana na ukwereketwa.
Kabul imekuwa inailaumu Pakistan kwa kuwaunga mkono, kichinichini, wapiganaji wa kitaliban, ambao Washington na Kabul wanadai kuwa wanatumia maeneo ya mpaka kama maficho yao.
Pia Karzai amekishutumu kikosi cha ujasusi cha Pakistan kwa kuhusika na mlipuko mkubwa wa bomu uliotokea katika ubalozi wa India mjini Kabul ambao uliwauwa watu 60.Pakistan ilikanusha kuhusika.