Karzai kuizuru India kuimarisha uhusiano
3 Agosti 2008New Delhi:
Rais Hamid Karzai wa Afghanistan anatarajiwa kuwasili India leo kuimarisha uhusiano na nchi hiyo, wiki chache tu baada ya hujuma ya bomu ya kujitoa mhanga kwenye ubalozi wa India mjini Kabul. Tukio hilo limezusha wasi wasi wa hali ya usalama katika kanda hiyo.
Afghanistan, India na Marekani zimelishutumu shirika la upelelezi la Pakistan, kuhusika na hujuma hiyo iliyowauwa watu 58 wakiwemo maafisa wawili wa ubalozi wa India. Pakistan imekanusha madai hayo.
Shambulio hilo lilikua ni pigo kwa utaratibu wa amani baiana ya India na Pakistan, uliozingatia jinsi Afhanistan inavyoweza haraka kugeuka kuwa chanzo cha mvutano wa kibalozi kati ya nchi hizo mbili.
Kwa upande mwengine Pakistan imekua na wasi wasi juu ya kuongezeka kwa ushawishi wa India nchini Afghanistan ambayo miaka ya karibuni imepokea mamilioni ya dola kama msaada wa maendeleo kutoka India.