1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kasheshe ya kulishwa sumu mpelelezi Skripal Magazetini

Oumilkheir Hamidou
5 Aprili 2018

Kasheshe ya shambulizi la sumu dhidi ya mpelelezi wa zamani wa Urusi, mkutano wa Syria na mjadala kuhusu hisia za chuki dhidi ya wayahudi ni miongoni mwa mada zilizochambuliwa magazetini hii leo.

UK Salisbury Untersuchung Nervengasanschlag Skripal
Picha: picture-alliance/PA Wire/B. Birchall

 

Tunazifungua kurasa za magazeti kwa tuhuma za kuhusika Urusi na kulishwa sumu mpelelezi Sergei Skripal na binti yake Julia. Licha ya visa kama hivyo kushuhudiwa mara nyingi katika miaka ya 90, hiki cha hivi karibuni kinazusha masuala kadhaa ya kuuliza. Gazeti la Weser-Kurier linaandika: "Kuna kadhia kadhaa za kuuliwa kiajabu ajabu wapelelezi na wakosoaji wa viongozi wa Kremlin nchini Uingereza. Katika miaka ya 90 tajiri mmoja wa Urusi alihujumiwa kwa sumu ya Nowitschok. Wakati ule simu yake ndiyo iliyokuwa imepakwa sumu. Katika kadhia ya Skripal, sumu inasemekana imepakwa mlangoni kwake. Ni dhana nzito hizo dhidi ya Moscow, lakini hakuna ushahidi. Wataalam wa shirika inalosimamia marufuku ya silaha za sumu wamechukua sampuli mahala tukio lilikotokea, wamechukua pia sampuli ya damu ya wahanga wa shambulio hilo. Walichokigundua kinaweza pengine kushadidia dhana hizo. Kremlin imeingiwa na wahka ndio maana wanashuku kama shirika hilo linaweza kuaminika. Kilichosalia ni kutaraji wahanga watazindukana siku moja na kueleza yaliyotokea-hata kama watalazimika kila siku kuhofia maisha yao."

 

Gazeti la "Südkurier" lina maoni kinyume na hayo na linaonya dhidi ya kumnyooshea kidole Putin bila ya ushahidi timamu: Gazeti hilo linaendelea kuandika:"Kushindana na Putin ni mchezo wa hatari na hasa unapohusika na upelelezi. Uingereza inajikuta katika hali hii wakati huu tulio nao. Waziri mkuu Theresa May amefanya pupa kuituhumu Moscow na ushahidi mpaka sasa bado hakupata. Hali hiyo inamrahisishia mambo Putin kushambulia na London kukabiliwa na dhana imetunga. Kinachotisha zaidi katika vuta nikuvute hii ni ule ukweli kwamba hakuna ajuaye lini, kiwingu kinachotanda katika anga ya mashariki na magharibi kitageuka dharuba. Hakuna atakaefaidika na hali hiyo na ndio maana wakati umewadia wa kurejea katika meza ya diplomasia."

Wadau wa vita vya syria wapigania masilahi yao

Mazungumzo ya pande tatu kati ya Urusi, Iran na Uturuki yamemulikwa pia na wahariri wa magazeti ya Ujerumani. "Stuttgarter Nachrichten" linazungumzia kuhusu mshikamano wa kijuu juu tuu. Gazeti hilo linaendelea kuandika: "Uturuki, Urusi, na Iran wanataka kujitokeza kama wadhamini wa utulivu katika vita vya Syria, lakini tofauti zao wanashindwa kuziweka kando. Sababu ni moja tu. Miaka saba tangu vita vilipoanza, wadau wote wanaamini wataimarisha nafasi zao katika uwanja wa vita na sio katika meza ya mazungumzo. Ushahidi wa hayo ni kujiingiza Uturuki kaskazini mwa Syria. Iran inaitaka Uturuki iikabidhi serikali ya Syria eneo la kaskazini la Afrin ililoliteka-viongozi wa mjini Ankara lakini wanapinga. Kutokana na hali hiyo mtu anaweza kusema juhudi za kisiasa za kumaliza mapigano hazina nafasi ya kufanikiwa."

Mjadala kuhusu hisia za chuki dhidi ya wayahudi

Mada yetu ya mwisho magazetini inatuwama katika mjadala wa hisia za chuki dhidi ya wayahudi. Kuna wanaohoji familia wapokonywe watoto wao ikiwa watawalea katika hisia kama hizo. Gazeti la "Südwest Presse" linaandika:"Bila ya shaka ni sawa kuhimiza hatua zaidi dhidi ya hisia za chuki dhidi ya wayahudi na hasa kutahadharisha dhidi ya hisia kama hizo miongoni mwa jamii ya Waislam nchini Ujerumani. Lakini hoja "kama watoto wakilelewa kwa misingi ya chuki dhidi ya wayahudi, watu wasichelee kuwaondowa katika familia zao, ni hoja ya hatari kwa ustawi wa mtoto na inafungamanishwa na masharti ya kila aina."

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandsapresse

Mhariri: Iddi Ssessanga

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW