Kashfa yaendelea kumuandama Fillon
13 Februari 2017Gazeti la Journal de Dimanche (JDD), limezikariri duru fulani zikisema tukio hilo litaashiria kwamba mwendesha mashtaka ameamua kutoifuta kesi hiyo, kwa kukosekana ushahidi ikiwa na maana ataendelea nayo.
Msemaji wa mwendesha mashtaka alisema hakuna uamuzi uliochukuliwa kwa wakati huu wala hakuna muda maalum uliowekwa, bali uchunguzi unaendelea.
Wakili wa Fillon na mke wake, hakutoa maelezo yoyote kuhusu matamshi hayo. Itakumbukwa Fillon, waziri mkuu wa zamani katika utawala wa Nicolas Sarkozy, amekiri kwamba mkewe alilipwa maelfu ya euro lakini anashikilia kazi aliyoifanya ilikuwa ni halali.
Fillon ambaye ameweza hadi sasa kukivuta chama chake upande wake, anapigania kuimarisha kampeni yake na kusema hatojitoa katika mbio hizo za urais, ikiwa utaanzishwa uchunguzi rasmi dhidi yake.
Utafiti wa maoni ya wapiga kura tangu ilipozuka kashfa hiyo karibu wiki tatu zilizopita, unaonyesha nafasi yake ya ushindi ikizidi kupunguwa.
Wapiga kura wamevunjika moyo kutokana na ripoti ya gazeti la kila wiki Canard Enchaine, kwamba mkewe alilipwa euro elfu kadhaa za walipa kodi kwa kazi ambayo huenda hata hakuifanya, kama mumewe alivyodai.
Awali ilionekana Fillon mwenye umri wa miaka 62, alikuwa na nafasi nzuri ya kushinda, lakini sasa ametupwa katika nafasi ya tatu katika duru ya kwanza ya uchaguzi Aprili 23, matokeo ambayo yatamuacha Marine Le Pen, kiongozi wa chama cha siasa kali za mrengo wa kulia, National Front, katika nafasi ya kwanza akifuatiwa na Emmanuel Macron, ambaye ni mgombe wa kujitegemea na hivyo wanasiasa hao wawili kuumana katika duru ya pili Mei 7.
Kwa mujibu wa Journal de Dimanche, kuna njia mbili zinazoweza kuchukuliwa na mwendesha mashtaka. Kwanza ni kuiwasilisha kesi hiyo kwa hakimu mchunguzi ambaye jukumu lake ni kuamua kama muhusika au wahusika wachunguzwe rasmi au njia ya pili itakuwa kesi hiyo kupelekwa moja kwa moja katika mahakama ya jinai.
Kama ni njia ya pili itakayotumika, gazeti hilo linasema, mchakato utaanza kwa uchache katika kiipindi cha siku 11.
Mgombea mbadala pindi Fillon atajiondoa
Pindi chama cha Republican kitahitaji kumteuwa mgombea mwingine mpya, siku ya mwisho ya kukusanya saini itakuwa Machi 17.
Kesi ya Fillon na malipo kwa mkewe, imetanuliwa na kuunganishwa na malipo yaliotolewa kwa wanawe wawili. Ofisi ya bunge ya mwanasiasa huyo imepekuliwa na watu wanne kuhojiwa na polisi.
Tayari watu wawili wanaoweza kujaza nafasi yake pindi atajitoa, wanaelekea hawako tayari kujaza pengo hilo. Alain Juppe, aliyetokeza nafasi ya pili nyuma ya Fillon wakati wa kura za mchujo, ameshatamka kuwa hana nia ya kuchukua nafasi hiyo na Nicolas Sarkozy aliyemaliza watatu na kutolewa katika duru ya kwanza ya mchujo, tayari iliamriwa mnamo Februari 7 afunguliwe mashtaka kutokana na kukiuka utaratibu wakati alipogombea muhula wa pili 2012 na kushindwa na Msoshalisti Francois Hollande. Sarkozy anasisitiza hana kosa lolote na mawakili wake wamesema watakata rufaa.
Majina mengine yanayotajwa na vyombo vya habari vya Ufaransa kujaza nafasi hiyo pindi Fillon atajitoa, ni pamoja na Rais wa Baraza la Seneti Gerard Larcher na mawaziri wawili wa zamani, Xavier Bertrand, na Francois Baroin.
Hata hivyo Baroin alisema mwishoni mwa juma, kwamba suala hilo halipo, kwani chama kina mgombea na wanamuunga mkono.
Utafiti mpya
Utafiti mpya wa wapiga kura, unaonesha mgombea wa National Front, Marine Le Pen, atapata asili mia 26 ya kura katika duru ya kwanza akifuatwa na Emmanuel Macron asilimia 22 na Fillon asilimia 21. Ikiwa duru ya pili itakuwa kati ya Le Pen na Macron, Macron atashinda kwa asili mia 63 kwa 37 .
Na pindi itakuwa ni Le Pen na Fillon, basi Fillon atashinda kwa asilimia 58 dhidi ya 42.
Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman/rtre
Mhariri: Yusuf Saumu