1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

KASHFA YA MARIFU NA BUNDESLIGA

11 Februari 2005

Ujerumani ina sifa ulimwenguni wa maandalio yake ya mashindano makuu kama vile michezo ya olimpik huko Munich, 1972,kombe la Dunia la dimba 1974 na hili lijalo 2006.Kila kitu kikenda barabara chini ya nahodha wa kamati ya maandalio ya kombe la dunia 2006-Franz Beckenbauer.

Ghafula wiki chache zilizopita, kukaibuka aibu ya rifu kupanga matokeo ya mechi walizochezesha ili kuvuna fedha kutoka makampuni ya mchezo wa kamari.

Hii imechafua heba ya Ujerumani na kuwatia wengine wasi wasi juu ya rifu watakaochezesha Kombe lijalo la dunia mwakani.Wengine wanakumbusha jinsi Ujerumani ilivyoshinda kwa kura moja tu dhidi ya Afrika Kusini kuandaa Kombe la mwakani la dunia.Utakumbuka Ujerumani iliipiku Afrika Kusini kwa kura 1 tu pale mjumbe wa New Zealand kinyume na maagizo ya shirikisho lake alipozuwia kutia kura yake na hivyo kura kuiangukia Ujerumani.Katika mkasa ule hukumu haikukatwa na marifu wala makampuni ya kamari,kinyume na kashfa hiiambayo inaelezwa ni kubwa tangu ile ya 1971.

Kashfa hii ya marifu Ujerumani imezifanya hata nchi jirani za Austria na Uswisi kuchukua hatua lakini pia UEFA-shirikisho la dimba la Ulaya limeamua sasa kutunga sheria kuzuwia mkasa uliozuka Ujerumani hauenei katika dimba nchi nyengine.

Mkasa huu lakini ulianza vipi na umefikia sasa umbali gani ?

Mkasa huu uliibuka hadharani Januari 22 mwaka huu.Tarehe hiyo, Shirikisho la dimba la Ujerumani (DFB) lilifichua kwamba halmashauri yake inayosimamia dimba inamchunguza rifu Robert Hoyzer. Tuhuma dhidi ya rifu Robert Hoyzer ni kwamba alipitisha udanganyifu katika mechi aliochezesha- kati ya SC Paderborn na Hamburg ya kuania Kombe la Taifa-DFB Pokal hapo August 28,mwaka jana.Rifu huyo alipangilia matokeo ya mechi hiyo ili avune kitita cha fedha katika mchezo wa kamari aliocheza.

Timu ya daraja ya tatu ya Paderborn kusema kweli, haingekua na nafasi kamwe kuwika mbele ya klabu ya Hamburg ya daraja ya kwanza ya Bundesliga.Lakini kwa mazingaombo ya rifu Robert Hoyzer uwanjani,SC Paderborn ilifanya maajabu na miujiza kwa kuilaza Hamburg mabao 4:2.Tena ilikua Hamburg ilioongoza kwa mabao 2 kabla chipikizi hao kutoka nyuma na kuwatoa nje ya Kombe hilo.

Rifu Hoyzer miongoni mwa visa vyake uwanjani ni kutoa mikwaju ya adhabu ya penalty dhidi ya hamburg pamoja na kumtoa nje Emile Mpenza, mchezaji wa Hamburg kutoka Ubelgiji wa asili ya Kongo.

Mwenyekiti wa Tume ya marifu ya Shirikisho la dimba la Ujerumani Theo Zwanziger alieleza hivi:

"kulikwishachomoza fununu fulani fulani kwamba mambo hayakwenda ipasavyo katika mechi hii na yanachunguzwa ambayo sasa kutokana na ushahidi mpya ulioibuka na tulio nao ,shaka shaka zilizokuwapo sasa zimepata nguvu."-alisema mwenyekiti huyo wa Tume ya marifu ya DFB.

Januari 24,rifu Ribert Hoyzer alikanusha wazi wazi kuwa alipitisha hadaa katika mechi aliziochezesha au alikua nazi.

Rifu Hoyzer:

"Si sawa kabisa yanayosemwa na naweza kukanusha tuhuma zote hizi."-alijitetea rifu Robert Hoyzer.

Klabu ya Hamburg ya Bundesliga ilionyimwa ushindi dhidi ya timu ya daraja ya tatu ya Paderborn ikatoa lalamiko rasmi kwa shirikisho la dimba la Ujerumani kuhusu jinsi rifu alivyochezesha mpambano ule na Paderborn.

Januari 26, shirikisho la kabumbu la Ujerumani likathibitisha taarifa la kuwapo gengi la Mafia wa wakroati linaloendesha biashara ya kamari kwa ujambazi.Taarifa kuhusu gengi hilo alitoa rifu Hoyzer.

Siku 2 baadae, yaani januari 27,mkasa huu wote ukaanza kuchukua sura nyengine ,kwani rifu Robert Hoyzer alianza kupasua hadharani na kuwataja wwaliokuwamo na wasio kuwamo.

Robert Hoyzer akifunua kawa alisema,

"Mnaweza kuelewa katika hali gani ya shinikizo niliojikuta siku hizi zilizopita.Nimefikiri sana na hata sikuweza kulala na hivyo sikuweza tzena kunyama kimya ......"

Mbele ya kituo cha Tv cha jiji la Berlin, rifu Robert Hoyzer akamwaga kila kitu na kutaja anayoyajua na nani waliohusika katika kamari na dimba nchini Ujerumani.

Januari 28,wakati akihojiwa rifu Robert Hoyzer aliungama kwamba alipokea kitita cha Euro 50.000 kwa kupangilia matokeo ya mechi alizochezesha.

Polisi mjini Berlin ikaanza msako wa m ajumba kadhaa na kati ya hayo mkahawa mmoja maarufu mjini Berlin ‘Cafe King’-shina la balaa lote hili.

Bw.Michael Grundwald kutoka afisi ya mshtaki mkuu wa serikali huko Berlin alisema,

"Jumla ya watu 4 wametiwa mbaroni.Wanashtakiwa ujambazi.Asakri 128 walishiriki katika msako na ushahidi umepatikana na sasa umo kufanyiwa tathmini."

Ilipoingia Januari 29,jarida la FOCUS liliripoti kuwa hata wachezaji 3 wa klabu ya HERTHA BERLIN ya Bundesliga ni miongoni mwa wanaotembelea mkaha wa huo wa CAFE KING-shina la kashfa hii.Nao walitajwa ni muangola Rafael,Madlung na mchezaji 3 Simunic .

Meneja wa klabu hii ya Bundesliga –hertha berlin-Dieter Hoeness akatangaza kuvichukulia hatua ya kisheria vyombo vya habari vinavyoeeneza habari hizo kuhusu wachezaji wake.Alidai hawakuhusika kabisa na ujambazi huo wa kupangilia matokeo na vituo vya kamari.

Januari 30, shirikisho la dimba la Ujerumani likamzuwia rifu mwengine –Jürgen Jansen asichezeshe mpambano wa Bundesliga baina ya Bremen –mabingwa na Hansa Rostock-ili kumlinda rifu huyo kama ilivyodaiwa.Siku moja baadae rifu huyo akala kiapo kwamba hakuhusika kabisa na ujambazi huo.

Februari mosi, magazeti kadhaa ya Ujerumani yaliripoti kwamba, rifu Hoyzer aliwaambia washtaki wa serikali kuwa rifu Jansen alipangilia matokeo mechi aliochezesha kati ya Kaiserslauten na Freiburg hapo Novemba mwaka jana.

Mkasa huu unaendelea kugubika kivuli chake katika dimba la Ujerumani.Kwani,umeshaanza kuwa mtindo rifu akipiga firimbi kuamua jambo ambalo shabiki wa timu fulani hakulipenda dhidi ya timu yake, anapaza sauti "Ah, wamekula mrungura hao".

Kwa jumla wachezaji 14 kutoka klabu zisizocheza katika Ligi ya Ujerumani-Bundesliga pia wanatuhumiwa kula fedha kutoka kwa mashabiki fulani wa timu zao ili kushawishi mkondo wa mchezo.

MAFIA ya wacroatia mjini Berlin,inadhaniwa kuhusika mno na kashfa hii ya kamari na dimba.

Heba na uaminifu wa marifu nchini humu imetetremka katika kashfa hii kubwa kabisa ya dimba tangu ile ya 1971.

Ujerumani inaanda mwakani Kombe la dunia na marifu wote watakaochezesha wataanza kukodolewa macho na uamuzi wowote watakaokata inapocheza timu ya Taifa ya Ujerumani na timu nyengine unaweza ukatiliwa shaka shaka-na hii ni mojawapo ya athari kubwa za kashfa hii kuzuka miezi 16 kabla kuanza kwa Kombe la dunia humu nchini.

Taarifa ziliibuka kwamba ujambazi wa aina hii kati ya vituo vya kamari na mchezo wa dimba unafanyika pia katika nchi jirani ya Austria.

Uswisi-pia jirani na Ujerumani, imeamua huko marifu waliopangwa kuchezesha mechi fulani,watatajwa siku ile ile ya mechi zenyewe na sio kabla. UEFA-shirikisho la dimba la Ulaya limeiarifu DFB-shirikisho la dimba la Ujerumani kwamba inatunga sheria mpya itakayowakataza marifu,wachezaji na viongozi wa dimba kutoacheza kamari.

Lakini ni kiasi gani cha fedha zinazoaniwa katika vituo vya kamari nchini Ujerumani ?

Soko la fedha kutoka kabumbu au spoti humu nchini ni nono kabisa.Kwa muujibu wa makisio yaliofanywa kila mwaka kima cha Euro bilioni 1.2 kinavunwa kutoka kamari ya spoti.Kampuni la kamari linaloongoza hapa ni lile la ODDEST,linalodhibitiwa na serikali.Yeyote atakae aweza kutia dau bni timu gani itashinda mweishoni mwa wiki hii katika Bundesliga.Katika soko hili kuna pia makampuni mengine 5 ya kamari ya kibinafsi ambayo yanaachiwa kuchezesha kamari ya mashindano ya mbio za farasi tu.

Kwa ufupi hakuna aibu au kashfa inayokaribishwa tena wakati wowote.Kuibuka lakini kwa kashfa hii miezi 16 kabla kuanza Kombe la dunia nchini Ujerumani ni bahati mbaya sana.Kwani,Ujerumani ilikua na azma ya kulitumia Kombe la dunia 2006 kujenga heba ya nchi hii.sasa lakini,limeandika gazeti mashuhuri la Ujerumani-DIE WELT- vyombo vya habari kuanzia nchini Marekani hadi Spain vinazungumzia sio dimba bali rushua na kashfa hii ya dimba.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW