Kashfa ya mtandao wa Facebook Zuckerberg kuhojiwa
5 Aprili 2018Taarifa hizo zimetolewa wakati ambapo maafisa wa bunge la Marekani wamefahamisha kuwa mkurugenzi mkuu wa mtandao wa Facebook Mark Zuckerberg atajibu maswali bungeni wiki ijayo juu ya kashfa iliyosababishwa na kampuni ya Cambridge Analytica iliyotumia data za watu kwa madhumuni ya kibiashara na kisiasa. Atafika mbele ya kikao cha pamoja cha kamati za biashara na sheria cha seneti ya Marekani.
Katika mahojiano na waandishi habari hapo jana Zuckerberg alikiri kwamba alifanya kosa kubwa sana kwa kushindwa kuangalia kwa undani wajibu wa Facebook duniani. Ameeleza kuwa haitoshi kwa mtandao wa Facebook kuwaamini watengenezaji wa App wanaposema kuwa wanafuata sheria. Zuckerberg amesisitiza kwamba Facebook inapaswa kuhakikisha watengenezaji hao wanazifuata sheria.
Mtandao wa Facebook unakabiliwa na kashfa kubwa kabisa kuwahi kutokea katika kipindi cha miaka mingi baada ya kuibuka madai kwamba kampuni ya Cambridge Analytica, inayohusiana na kampuni ya data ya Trump, ilitumia taarifa za mamilioni ya watumiaji wa mtandao wa Facebook kwa ajili ya kushawishi chaguzi. Taarifa hizo zilizopatikana kwa njia haramu zilipitishwa kwenye App.
Facebook imesema watumiaji wa mtandao huo wapatao milioni 87 huenda walikumbwa na hujuma hiyo. Huenda data zao zilitumiwa. Kwa mujibu wa taarifa, hilo ni ongezeko la watumiaji milioni 50. Facebook imefanya tathmini hiyo kutokana na idadi ya marafiki ambao kila mtumiaji alikuwa nao.Lakini kampuni ya Cambridge Analytiya imesema ilitumia data za watu milioni 30 tu. Hata hivyo hapo jumatatu ijayo watumiaji wa Facebook watapata fursa ya kuamua ni Apps zipi wanatumia na habari zipi walizobadlishana kwa kutumia Apps hizo. Watukuwa na uwezo wa kuzifuta Apps ambazo hawazihitaji. Watumiaji waliokuwa na data walizoziweka wazi kwa kampuni ya Cambridge Analytica watapewa taarifa hiyo. Facebook imeeleza kuwa idadi kubwa ya watumiaji walioathirika ni wale wa nchini Marekani. Hata hivyo mkurugenzi mkuu wa Facebook Zuckerberg amesema itachukua muda wa miaka mingi ili kuweza kuyatatua matatizo yaliyotokea.
Mbali na kashfa ya kutumiwa data za faragha za wateja, Facebook pia imekuwa inakabiliana na tatizo la taarifa za uongo, kutumiwa kwa mtandao huo kwa ajli ya kueneza chuki na uchochezi na pia wasiwasi juu ya athari za mitandao ya kijamii katika akili za watu. Bwana Zuckerberg amesema masuala hayo ni muhimu na pia yanawakilisha mabadiliko makubwa wakati ambapo Facebook inapanuza wigo wa wajbu wake. Ameeleza matumaini kwamba hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu kampuni yake itakuwa imeleta mageuzi makubwa juu ya masuala mengi.
Mkurugenzi huyo amejitwika binafsi jukumu la kuyatatua matatizo ya kampuni hiyo mnamo mwaka huu. Pamoja na hatua kadhaa zitakazochukuliwa na kampuni ya Facebook ni kupunguza upatikanaji wa data za watu kwa njia ya Apps na pia itazuia upatikanaji wa habari juu ya makundi, kama vile orodha za wanachama na maudhui.
Hatua nyingine muhimu itakayochukuliwa ni kuwataka watumizi wanaofanya utafiti kujulisha namba zao za simu au anuani za barua pepe. Wakati njia hiyo hapo awali ilisaidia watu kuwasiliana na marafiki, makampuni yaliyokuwa na namba za simu na anuani za barua pepe za watu yaliweza kukusanya habari juu yawateja.
Facebook imesema inaamini kwamba habari juu ya wateja wao bilioni 2.2 zilitumiwa na makampuni na watu wengine wabaya. Mawasiliano na maudhui yaliyokusudiwa kuonekana kwa marafiki tu yalikusanywa na watuhao wabaya na makampuni. Hapo jana Facebook ilizindua sera mpya inayofafanua taratibu za ukusanyaji na matumizi ya data.
Mwandishi:Zainab Aziz/APE
Mhariri: Iddi Ssessanga