Kashfa ya upelelezi yaitikisa Deutsche Bahn
29 Januari 2009Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wamemulika zaidi kisa cha upelelezi katika shirika la usafiri wa reli-Deutsche Bahn na tangazo la Urusi la kutotega makombora angalao kwa sasa katika eneo la Kaliningrad.Mbali na mada hizo, wahariri wamechambua pia maelezo ya kiongozi wa kanisa katoliki ulimwenguni Papa Benedikt wa 16 kuhusiana na kubatilishwa amri ya kutengwa maaskofu wanne.Tuanze lakini na kisa cha upelelezi katika shirika la usafiri wa reli Deutsche Bahn.Gazeti la Berliner Zeitung linaandika:
"Katika miaka ya nyuma shirika la usafiri wa reli la Ujerumani-Deutsche Bahn,liliamuru wapelelezwe watumishi wake wasiopungua laki moja na 73 elfu,kwa dhana za kuhusika na rushwa.Kwa maneno mengine idadi hiyo ni sawa na robo tatu ya wafanyakazi jumla waliokua wakichunguzwa.Idadi hiyo ya watu pekee inamfanya mtu mwili umsisimke."
Hayo ni maoni ya BERLINER ZEITUNG,nalo gazeti la FRANKFURTER RUNDSCHAU linaandika:
Upelelezi kwa mtindo wa Deutsche Bahn dhidi ya ushirika wa wahalifu waitwao wafanyakazi.Kuna mengi ya kusema kuhusu shirika hilo na mitindo yake.Picha inayojitokeza ni ile ya shirika lisilowaamini watumishi wake na kuwadhania wote kua ni wahalifu."
Nalo gazeti la BRAUNSCHWEIGER ZEITUNG linaandika:
Kati ya zaidi ya watumishi laki moja na 70 elfu elfu waliochunguzwa,mia moja tuu ndio waliokutikana na hatia ya rushwa.Huo ni ushahidi tosha kwamba,idadi kubwa ya madareva wa reli,mafundi na watumishi wa idara za utawala wanafanya kazi zao kama inavyostahiki.Si hasha kwa hivyo wakiangalia hatua za upelelezi dhidi yao kua ni tusi.
Gazeti la MITTELDEUTSCHE ZEITUNG la mjini Halle linachambua taaarifa ya Urusi ya kuzuwia angalao kwa sasa kutega makombora yake katika ardhi ya Kaliningrad:Gazeti linaandika:
Kufumba na kufumbua kila kitu kinaonyesha kubadilika:Marekani haitoi tena kipa umbele kwa mipango ya kutega makombora ya kinga barani ulaya ,na Urusi nayo inaachana na mpango wake wa kutega makombora ya masafa mafupi katika eneo la Kaliningrad.Kitisho cha kuanza upya mbio za kujirundikia silaha kimepwaya hata kabla ya hatua zozote kuchukuliwa.Hali hiyo ni ya maana,hasa kwa Ulaya.Kwasababu pekee fikra ya kutegwa makombora hayo imechafua uhusiano wa pande mbili ,ingawa hakujakua na uhakika wowote kama yangetumiwa.Na sio pekee uhusiano kati ya Washington na Moscow,bali hata miongoni mwa nchi za Ulaya wenyewe kwa wenyewe."
Gazeti la SÜDDEUTSCHE ZEITUNG linaandika:
"Kila upande unatambua,kuna la muhimu zaidi kuliko kuendelea na ushari wa miezi ya nyuma.Mzozo wa kiuchumi unaigubika Marekani na Urusi pia kwa hivyo hakuna wakati wa kujishughulisha na miradi isiyokua na maana na yenye kugharimu mafedha chungu nzima."