1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

kashfa zazidi kumuandama Trump

Sekione Kitojo
17 Mei 2017

Rais Donald Trump binafsi  alimtaka  mkurugenzi wa zamani  wa shirika la FBI nchini Marekani James Comey kuachana na uchunguzi kuhusiana na mshauri  wa usalama wa taifa Michael Flynn.

USA Treffen zwischen Trump und Lavrov
Rais Trump (katikati) alipokutana na waziri wa kigeni wa Urusi Lavrov na balozi wa Urusi nchini Marekani Sergei KislyakPicha: picture alliance/dpa/A. Shcherbak

Ikulu  ya  Marekani  ya White House  ilikana  vikali  baada  ya  dondoo  hizo  kuwekwa  wazi baadaye  jana, mwishoni  mwa  siku iliyokuwa  na  heka  heka  nyingi za  kupambana  na  ripoti  zilizoonekana  kuwa  na  madhara makubwa tangu mapema  kwa utawala  huo.

Mkurugenzi wa zamani wa FBI James ComeyPicha: Reuters/K. Lamarque

Taarifa  hizo  kutoka  kwa  James Comey  zimekuja  wakati  utawala huo  uliojiingiza  katika  matatizo  ulikuwa  bado  unahangaika  kutoa maelezo  kuhusu  taarifa  zilizojitokeza  kwamba  rais  alitoa  taarifa nyeti  kwa  waziri wa  mambo  ya  kigeni  wa  Urusi  pamoja  na balozi  wa  nchi  hiyo  nchini  Marekani. Wakitetea  hatua  za  Trump , maafisa  walipuuzia  umuhimu   na  usiri  wa  taarifa  hizo, ambazo ziliwasilishwa  na  Israel chini  ya  makubaliano  ya  kubadilisha taarifa  za  kijasusi, na  Trump  binafsi  amesema  ana  haki  zote, kama  rais  kubadilishana  taarifa  hizo  zinazohusu  ugaidi  na usalama  wa  safari  za  anga  na  Urusi.

Pamoja  na  hayo  washirika  wa  Marekani  na  baadhi  ya  wajumbe wa  baraza  la  Congress wameeleza  wasi  wasi wao  unaokaribia kuwa  tahadhari. Seneta  kutoka  chama  cha  Republican  John McCain  ametoa  matamshi  makali  jana kuwahi  kutolewa  na kambi  ya  chama  cha  Republican. Licha  ya  kwamba  hata  baada ya  jana  kutolewa  taarifa  hiyo, wajumbe  kutoka  chama  hicho walisita  kumkosoa  rais, licha  ya  kwamba  mbinyo  wa  kujitokeza kufanya  hivyo  ukiongezeka. McCain  amesema  hali  hii  sasa imekaribia  kiwango  cha kashfa  kubwa  ya  Watergate.

Seneta wa Marekani John McCainPicha: picture-alliance/dpa/M. Balk

"Kitu ninachoweza  kusema  ni  kwamba  tuliisha  ona  filamu  hii hapo kabla. Nafikiri  inafikia  katika  kiwango  ambapo  ni  sawa  na Watergate na  viwango vya  kashfa  nyingine  ambazo  mimi  na wewe  tumekwisha  shuhudia. Ni kama jongoo  mwenye miguu  mingi , na kwamba  kila  mara kiatu kikitoka  mguuni  kila  baada  ya  siku kunaonekana  upande  mwingine  wa  hali  hii  isiyofurahisha."

Kwa upande  wa  Comey  binafsi  ambaye Trump  alimfuta  kazi  wiki iliyopita, mkurugenzi  huyo  wa  shirika  la  FBI  aliandika  katika kumbukumbu  baada  ya  mkutano  wa  mwezi  Februari  katika  Ikulu ya  White  House  kwamba  rais  mpya  amemuomba  kufunga uchunguizi  wa  shirika  hilo  kumhusu  Flynn  na  mawasiliano   yake na  Urusi, amesema  mtu  aliyesoma  kumbukumbu  hizo. Uchunguzi kuhusu  Flynn   ulikuwa  sehemu  ya  uchunguzi  mpana  zaidi kuhusiana  na  Urusi  kuingia  uchaguzi  wa  rais  mwaka  jana.

Aliyekuwa mshauri wa masuala ya usalama wa taifa nchini Marekani Michael FlynnPicha: picture-alliance/AP Photo/C. Kaster

Mbunge  wa  baraza  la  wawakilishi Jason Chaffetz , mwenyekiti  wa kamati  ya   bunge  kutoka  chama  cha  Republican , ametuma barua  kwa  shirika  la FBI  jana  Jumanne  inayoomba  kwamba shirika  hilo liwasilishe  nyaraka  zote  na  sauti zote  zilizorekodiwa ambazo  zinaeleza  kuhusu  mawasiliano  kati ya  Comey  na  Trump. Amesema anaipa shirika  la  FBI wiki  moja  na  kama  tutahitaji kushitaki  tutafanya  hivyo.

Mwandishi: Sekione Kitojo / ape

Mhariri:  Yusuf Saumu

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW