Kaskazini mwa Mali kwaanza kutulia
16 Januari 2013Waislamu wenye itikadi kali wanaojiita walinzi wa dini, Ansar Dine, waliudhibiti mji wa Gao kaskazini mwa Mali kwa muda wa nusu mwaka. Baada ya kuwatimua washirika wao wa hapo awali, waasi wa Tuareg, wapiganaji wa Ansar Dine walianza kuzitumia sheria za Kiislamu.
Lakini sasa watu katika mji wa Gao na mingine ya kaskazini mwa nchi hiyo wameanza kupata utulivu baada ya wapiganaji hao wa Kiislamu kutimua mbio kufuatia mashambulizi ya ndege za Ufaransa.
Licha ya hisia za faraja kuonekana miongoni mwa wakaazi hao wa kaskazini, hata hivyo watu hao pia wana wasiwasi, kwa sababu mgogoro wa nchi yao bado haujamalizika licha ya hatua za kijeshi zinazochukuliwa na Ufaransa.
"Sasa hali ni shwari. Watu wanatoka majumbani mwao kuvuta sigara nje bila ya usumbufu. Hata hivyo, muda mfupi uliopita ndege zilishambulia karibu na hapa. Lakini hakuna raia yeyote aliyedhurika. Baadhi ya wapiganaji wa Kiislamu bado wapo, lakini hawatoki nje ya magari yao," anasema mmoja wa wakaazi hao.
Mchanganyiko wa faraja na shaka
Watu wamevuta upumzi wa faraja katika mji wa Sevare uliopo kusini mwa Mali. Mji huo upo kwenye mpaka na sehemu ambayo hadi sasa inadhibitiwa kikamilifu na Waislamu wenye itikadi kali.
Endapo waasi wangelifanikiwa kufika hadi kwenye kituo cha majeshi ya serikali, katika mji mkuu wa jimbo hilo, Mopti ,basi ingekuwa rahisi kwao kufika haraka katika mji mkuu wa Mali, Bamako.
"Niligwaya hadi tumboni wiki jana baada ya waasi kuuteka mji wa Konna. Kwani kutoka hapa hadi mji huo ni umbali wa kilometa 70 tu." Anasema Besema mmoja wa wakaazi wa Mopti, alieongeza kuwa wamepumua kidogo baada ya kusikia kwamba waasi wa Kiislamu wamerudi nyuma.
"Watu sasa wametulia na wamechangamka. Baada ya waasi kurudi nyuma,watu walifikiri vita vimekwisha. Waasi ni hadori sana kwa kujificha. Wanaingia vichakani ili kuepuka kuonekana mijini. Na ghafla tu wanaibuka katika sehemu nyingine."
Wakimbiao si waasi pekee
Lakini mashambulizi ya Ufaransa dhidi ya wanamgambo wa Ansar Dine hayawakimbizi waasi hao tu, bali raia wa kawaida ambao wanayahama makaazi yao kwa kiwango kikubwa kuhofia kukutwa katikati ya mapigano.
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wakimbizi wa Mali nchini Niger, Seydou Amadou Cisse, ameeleza kuwa sasa pana msongamano mkubwa wa wakimbizi na anafikiri wimbi kubwa la wakimbizi bado linakuja, huku Umoja wa Mataifa ukikadiria idadi ya wakimbizi kufikia 30,000.
Mwandishi: Hille Peter/DW Afrika
Tafsiri: Abdu Mtullya
Mhariri: Iddi Ssessanga