1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Katiba mpya Kenya kama kielelezo cha uhuru

12 Desemba 2013

Wakati katiba ya Kenya ilipokuwa inatangazwa rasmi katika Uwanja wa Uhuru mwaka wa 2010, ilikuwa moja ya mafanikio muhimu yaliopatikana nchini humo tangu kunyakuliwa uhuru mwaka wa 1963.

Wapigakura nchini Kenya wakionesha kura zao katika kura ya maoni ya katiba mpya mwaka 2010.
Wapigakura nchini Kenya wakionesha kura zao katika kura ya maoni ya katiba mpya mwaka 2010.

Hatua ya kuzindua katiba hiyo iliopewa jina la "Uzinduzi wa Jamhuri ya Pili ya Kenya" ilipita baada ya kupata asilimia 67 ya kura kufuatia Wakenya kuipitisha katika kura ya maoni ya Agosti 4.

Wakenya walikuwa na furaha kubwa sana ya kupata katiba baada ya miaka 20 ya kuhangaika. Waliiunga mkono kwa kiwango kikubwa wakitumai serikali imepata hati itakayoweza kutoa muongozo wa namna ya kuendesha taifa kwa mfumo wa kidemokrasia.

Katiba ya zamano ililaumiwa sana kwa kuendeleza mfumo duni wa kuendesha shughuli za serikali, ukabila, kutoa nafasi ya kutodhibiti kwa umakini mali za serikali na pia kuwepo kwa nafasi ya watu kukwepa mkono wa sheria.

Changamoto katika Katiba Mpya

Wapigakura wakisubiri kupiga kura zao katika kura ya maoni ya katiba mpya mwaka 2010 nchini Kenya.

Japokuwa Kenya ilitoa mfano wa kuigwa katika eneo hilo la Afrika kwa kujipatia katiba inayoangazia pia haki za binaadamu, utekelezwaji wake umetoa changamoto kubwa katika taifa hilo. Kumekuwa na vuta nikuvute kati ya ofisi ya mkuu wa sheria na kamisheni iliyofanyia marekebisho katiba hiyo (CIC) inayoongozwa na Charles Nyachae.

Kamisheni ya CIC imekuwa ikitoa lawama kwamba afisi ya mkuu wa sheria inachukua muda mwingi sana katika kuchapisha miswada na kuiwasilisha kwa baraza la mawaziri na bunge.

Moja ya changamoto nyingi zilizokuwepo pia ni kwamba wengi wa wabunge hawakuwa na ufahamu zaidi wa masuala mengi yaliokuwa katika katiba hiyo mpya.

Wanadaiwa kutafsiri vibaya baadhi ya vipengele aidha kwa makusudi au kwa bahati mbaaya lakini kwa namna ambayo itawafaidisha wabunge wenyewe kwa upande wa kisiasa.

Vile vile, baadhi ya maafisa katika serikali ya Kenya waliokuwa wanapinga katiba hiyo walifanya juu chini kujaribu kuiangamiza katiba mpya.

Walijaribu kila wawezalo kupenyeza vipengele vya katiba iliyopita katika katiba mpya ili kukidhi mahitaji yao binafsi.

Hata hivyo, katiba hiyo ilifanikiwa kuandikwa na kupigiwa kura ya maoni na raia wa Kenya na kupitishwa kwa asilimia kubwa baada ya kuisoma na kuielewa.

Kwa sasa changamoto kubwa iliopo ni kutekelezwa kwa baadhi ya vipengele viliyoopo katika katiba hiyo.

Imetafsiriwa na Amina Abubakar
Chanzo: The Daily Nation (Kenya)
Mhariri: Mohammed Khelef

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi