Katiba mpya yaelekea kukubalika Kenya
5 Agosti 2010Kenya, inaelekea kuikubali katiba mpya baada ya matokeo ya awali ya kura ya maoni iliyopigwa jana ya kuikubali ama kuikataa katiba hiyo, kuonesha kwamba zaidi ya theluthi mbili ya kura zilizopigwa katika kura hiyo ya maoni zinapendelea katiba mpya.
Kura zaidi ya milioni sita ambazo zimehesabiwa hadi kufikia saa sita ya usiku, zimeonesha kuwa asilimia 66.9 wamepigia kura ya ndio kutaka katiba mpya, huku matokeo kamili yakitarajiwa kutangazwa baadaye leo, mara tu kura zote zitakapohesabiwa.
Nao waangalizi wa zoezi hilo wamesema wameridhishwa mwenendo mzima wa upigaji kura na kutaka utulivu wakati kura hizo zikiendelea kuhesabiwa.
Zoezi hilo la upigaji kura lilifanyika jana kwa amani na utulivu katika maeneo yote nchini humo.
Jumla ya watu milioni 12.5 walijiandikisha kupiga kura.
Katiba hiyo mpya ina lengo la kupunguza madaraka ya rais na kuwapa haki zaidi raia.
Kambi ya wanaoiunga mkono katiba hiyo inaongozwa na Rais Mwai Kibaki na Waziri mkuu Raila Odinga.