Katibu mkuu wa NATO Rutte kukutana na Trump
8 Aprili 2026
Kwanza katibu mkuu huyo wa Nato anakutana na waziri wa mambo ya nje Marco Rubio kabla hapo baadae hivi leo kukukatana na Trump kwenye kikao ambacho kinakuja baada ya Marekani na Iran jana kukubaliana kusitisha mapigano kwa wiki mbili pamoja na kufunguliwa tena kwa njia muhimu ya bahari ya Hormuz.
Usitishaji vita ulianza baada ya Trump kusema kwamba angeshambulia vinu vya nyuklia vya Iran na madaraja na pia kutishia kusambaratisha kila kitu nchini humo.
Mpango wa kufungua mlango huo wa bahari unatarajiwa kuwa kipaombele cha mkutano huo wa leo alasiri.
Rutte na Trump watarajiwa kukutana hadharani
Ikulu ya White House imesema mkutano huo unatarajiwa kufanyika faraghani, lakini katika utawala wa Trump, hilo linaweza kubadilika dakika ya mwisho, na kuwa wazi kwa waandishi wa habari.
Vyanzo viwili vya kidiplomasia vya Ulaya, vimesema wakati viongozi hao wawili watakapokutana, Rutte huenda akaonyesha nia ya pamoja ya kudumisha biashara ya kawaida ya baharini baada ya uhasama kusababisha kupanda kwa bei ya nishati kote duniani.
Pia anatarajiwa kumshawishi kiongozi huyo Marekani kuacha ukosoaji wa umma dhidi ya muungano huo, huku akipigia debe hatua ambazo nchi za Ulaya zinachukua kuongeza matumizi katika sekta ya ulinzi.
Afisa mmoja wa NATO amesema Rutte atatafuta kuongeza ushirikiano wa sekta ya ulinzi na kujadili vita nchini Iran na
Ukraine. Lakini haijajulikana ikiwa NATO, muungano unaolenga Amerika Kaskazini na Ulaya, utatekeleza jukumu kubwa katika Mashariki ya Kati.
Kulingana na mmoja wa wanadiplomasia hao, Rutte hajapewa jukumu na viongozi wa Ulaya kujitolea kufanya operesheni katika Mlango-Bahari wa Hormuz atakapokutana na Trump.
Seneta wa Republican aiunga mkono NATO
Jana jioni, Seneta Mitch McConnell wa chama cha Republican kutoka Kentucky, alitoa taarifa iliyounga mkono muungano huo wa NATO na kusema kufuatia mashambulizi ya Septemba 11, washirika wa NATO walituma wanajeshi wao kupigana pamoja na wale wa Marekani nchini Afghanistan na Iraq.
McConnell, ambaye ni mwanachama wa kamati inayosimamia matumizi ya ulinzi, amemhimiza Trump kuwa "wazi na thabiti" na kusema sio nia ya Marekani kutumia muda mwingi kuwawekea kinyongo washirika wanaojali masilahi yake badala ya kukabiliana na wapinzani wanaowatishia.
Ikiwa mkutano wa Rutte hautapunguza mvutano na Trump, haijulikani ikiwa serikali ya Trump itapinga sheria inayomzuia rais kujiondoa katika NATO bila idhini ya bunge. Sheria hiyo ilipopitishwa, iliungwa mkono na waziri wa mambo ya nje wa sasa wa Trump, Marco Rubio, ambaye wakati huo alikuwa seneta kutoka Florida.