NATO kumshawishi Trump juu ya mkataba wa silaha kwa Ulaya
9 Januari 2025Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO, Mark Rutte amesema Alhamisi kuwa anafanya juhudi kumshawishi Rais mteule wa Marekani Donald Trump, kupunguza vizuizi vya upatikaji wa mifumo ya silaha za Marekani kwa washirika wa Ulaya.
Rutte ameliambia shirika la habari la dpa kwamba washirika wa Ulaya tayari wamewekeza mabilioni ya dola katika sekta ya ulinzi ya Marekani.
Hata hivyo, Katibu Mkuu huyo wa NATO anaamini kwamba wanaweza kupata mafanikio makubwa zaidi iwapo sekta ya ulinzi ya Marekani itakuwa huru zaidi, kwa kuondoa idhini ya Bunge la Marekani, wizara ya ulinzi, Pentagon na Ikulu ya White House.
Ametolea mfano wa mahitaji ya Ulaya ya mfumo wa ulinzi wa anga chapa Patriot uliyochukua muda mrefu kufika Ulaya. Trump kwa muda mrefu amezikosoa nchi wanachama wa NATO kwa kutowekeza zaidi katika sekta ya ulinzi na badala yake wakitegemea ulinzi wa Marekani.