1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa azuru bandari ya Odessa.

Zainab Aziz Mhariri: Grace Patricia Kabogo
19 Agosti 2022

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amezuru bandari kuu ya Odessa inayokabiliwa na vita kusini mwa Ukraine na ameitaka Urusi isikate umeme kwenye kinu cha nishati ya nyuklia cha Zaporizhzhia.

Ukraine | UN Generalsekretär Antonio Guterres in Odessa
Picha: BULENT KILIC/AFP/Getty Images

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio uterres leo ametoa mwito huo kwamba kinucha nyuklia cha Zaporizhzhia kinachokaliwa na Urusi kisikatiwe umeme kutoka kwenye gridi ya taifa ya Ukraine, kufuatia ripoti za Ukraine kwamba Moscow inapanga kufanya hivyo.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameyasema hayo katika ziara yake kwenye bandari ya Odessa kusini mwa Ukraine. Ziara hiyo ya Guterres inafanyika siku moja baada ya Katibu mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa kusema harakati za kijeshi katika eneo la karibu na kinu cha nishati ya nyuklia cha Zaporizhzhia lazima zisimamishwe haraka. Aliyasisitiza hayo katika mazungumzo ya mjini Lviv alipokutana na marais wa Ukraine, Volodymr Zelensky na mwenzake wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan hapo jana Alhamis.

Kushoto: Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan. Katikati: Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy. Kulia: Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres.Picha: Evgeniy Maloletka/AP/picture alliance

Guterres alisema: "Nina wasiwasi mkubwa kuhusu hali inayoendelea ndani na karibu ya kinu kikubwa zaidi cha nishati ya nyuklia barani Ulaya cha Zaporizhzhia. Busara lazima itumike ili kuepuka vitendo vyovyote vinavyoweza kuhatarisha usalama wa watu na wa kinu hicho cha nyuklia. Eneo hilo halipaswi kutumika kama sehemu ya operesheni yoyote ya kijeshi. Badala yake, makubaliano yanahitajika kwa haraka ili kuirejesha Zaporizhzhia katika hali ya  miundombinu ya kiraia na kuhakikisha usalama wa eneo hilo."

Kinu hicho cha Zaporizhzhia kikubwa zaidi cha nyuklia barani Ulaya kinachodhibitiwa na Urusi kilicho karibu na Rasi ya Crimea kina uwezo wa kusambaza umeme kwa takriban nyumba milioni nne. Kupamba moto kwa mapigano karibu na kinu hicho kumesababisha viongozi wa dunia kutoa onyo na tahadhari akiwemo Guterres ambaye amesema uharibifu wowote kwenye kinu hicho utakuwa sawa na kujiua.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres.Picha: Yuki Iwamura/AP/dpa/picture alliance

Guterres pia amesema Uturuki imefahamisha kuwa Ukraine inajiandaa kurefusha mkataba wa kihistoria wa kusafirisha nafaka uliofikiwa pamoja na Urusi. Tangu makubaliano hayo kufikiwa meli 25 zilizobeba takriban tani 600,000 za bidhaa za kilimo zimeondoka kutoka kwenye bandari tatu zilizoteuliwa kwa mujibu wa Ukraine.

Soma zaidi:Viongozi wa UN, Uturuki, Ukraine wajadili njia za kumalizia vita vya Urusi

Guterres anatarajiwa kuelekea Uturuki baada ya ziara ya Odessa ambako atakitembelea Kituo cha Uratibu wa Pamoja, kilichopewa jukumu la kusimamia makubaliano hayo. Makubaliano kati ya Ukraine na Urusi ya kufungua njia kutoka bandari tatu za Ukraine, ikiwemo ya Odessa, yameleta afueni na kupunguza wasiwasi wa kuwepo uhaba wa chakula duniani wakati ambapo nchi hizo mbili zinazopigana ni miongoni mwa wazalishaji wakuu duniani.

Mashambulio katika eneo la DonbasPicha: Aris Messinis/AFP

Wakati hayo yakiendelea vikosi vya Urusi vinaendeleza mashambulizi ya mabomu katika eneo la mashariki mwa Ukraine la Donbas, huku Kyiv ikiripoti kuwa watu watano wameuawa katika jimbo la viwanda la Donetsk katika muda wa saa 24 zilizopita.

Vyanzo:/AFP/p.dw.com/p/4FkXe

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW