Katumbi: Tshisekedi ameshindwa kuleta utulivu Kongo
24 Novemba 2023Baada ya kuzindua kampeni zake za uchaguzi mjini Kisangani na katika mkoa jirani wa Ituri, Katumbi amelaani pia uzembe wa mamlaka katika kushughulikia hali ya usalama mashariki mwa nchi hiyo .
Akiwa ameandamana na washirika wake wapya, wakiwemo waziri mkuu wa zamani Augustin Matata Ponyo, Seth Kikuni na Frank Diongo, Moise Katumbi alilakiwa na maelfu ya wafuasi ambao hawakuruhusiwa kuingia ndani ya uwanja wa ndege wa kimataifa mjini Goma kabla ya ndege yake kutua.
Pamoja nakumuunga mkono, raia hao waliokuwa wakibeba bendera za chama cha Ensembele pour la Republique kinacho ongozwa na tajiri huyo ambaye pia ni Gavana wa zamani wa jimbo la katanga, walionesha pia hasira yao baada yakuzuiliwa na jeshi polisi kumkaribisha kiongozi wao.
Soma pia:Wagombea sita wa urais kongo waitaka mahakama ya juu kuhakikisha uchaguzi wa haki
Wakati wa mkutano wa hadharani uliofanyika jana Alhamisi jioni, Moise KATUMBI mgombea wa uchaguzi wa Urais wa desemba 20, aliahidi kurejesha usalama katika mikoa ya Ituri na kivu kaskazini,inayoyumbishwa na vita kwa sasa.
Changamoto ya ajira kwa vijana Kongo
Kwa takriban dakika 60, mgombea huyo ambaye uraia wake unaendelea kuzua utata nchini Kongo, alikosoa kwa nguvu rekodi ya utawala wa sasa, akilaani kuendelea kwa ukosefu wa ajira kwa vijana pamoja na mishahara duni kwa askari wanaokabiliana na makundi ya waasi kila uchao.
Wakati huo huo, kundi jengine la vijana waliandamana upande wa mashariki mwa mji wa Goma wakitaka kuzuiliwa kwa Katumbi kuingia mjini Goma wakimtuhumu kutolitaja taifa la Rwanda kuunga mkono waasi wa M23 katika vita vinavyoendelea sehemu mbalimbali hapa kivu kaskazini.
Soma pia:Kuondolewa vipeperushi vya wagombea kunazusha mvutano Kongo
Hata hivyo, wakati kampeni za uchaguzi zikiendelea, baadhi ya wagombea urais wanakosoa ukiukwaji wa taratibu katika mchakato wa uchaguzi.
Wagombea sita ambao ni Martin Fayulu, Floribert Anzuluni, Theodore Ngoy, Nkema Liloo pamoja na Jean-Claude Baende wametishia kuwasilisha malalamiko yao mbele ya mahakama makuu wakimshtaki kiongozi wa tumehuru ya uchaguzi pamoja na waziri wa mambo ya ndan kwa ukiukwaji huo.