1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani

Kauli za Trump zakemewa vikali na viongozi duniani

Saleh Mwanamilongo
8 Januari 2025

Rais mteule wa Marekani, Donald Trump, amezuwa mjadala mkali kimataifa baada ya kutaja uwezekano wa kuuchukuwa Mfereji wa Panama, kisiwa cha Greenland na kuigeuza Canada kuwa jimbo la 51 la Marekani.

Trump azusha tafrani akitaka kuzichukuwa Greenland, Canada na Mfereji wa Panama
Trump azusha tafrani akitaka kuzichukuwa Greenland, Canada na Mfereji wa PanamaPicha: Evan Vucci/AP/picture alliance

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Florida, Donald Trump amesema hawezi kuondosha uwezekano wa kutumia nguvu za kiuchumi au kijeshi kutwaa udhibiti wa Mfereji wa Panama na kisiwa cha Greenland.

Trump alikosowa vikali utumiaji wa bidhaa za Canada na pia msaada wa kijeshi wa Marekani kwa jirani yake huyo, akidai mpaka baina yao ni wa kubuni. Kuhusu Greenland, kisiwa chenye utajiri wa rasilimali kinachomilikiwa na Denmark, Trump alisema atatumia shinikizo la kiuchumi ikiwa Copenhagen itakataa kuiuzia Marekani kisiwa hicho.

"Wote watakuwa wakibadilisha jina la Ghuba ya Mexico hadi Ghuba ya Amerika, ambayo ina mzunguko mzuri unayofunika eneo kubwa. Ghuba ya Amerika. Ni jina zuri. Na linafaa. Na Mexico inapaswa kuacha kuruhusu mamilioni ya watu kuingia nchini mwetu. Wanaweza kuwazuia.", alisema Trump.

Kabla ya kuendelea kusema : "Na tutaweka ushuru mkubwa sana kwa Mexico na Canada kwa sababu wahamiaji wanapitia pia Canada. Na dawa za kulevwa ambazo zinaingia ziko kwenye viwango vya juu."

Ufaransa yaonya vitisho dhidi ya mipaka huru ya Ulaya

Ufaransa imemuonya Donald Trump dhidi ya kile ilichokiita kuwa ni kutishia "mipaka huru" ya Umoja wa UlayaPicha: Julien de Rosa/AFP

Waziri Mkuu wa Canada, Justin Treudau, amemkosowa vikali Trump kwa kauli yake hiyo, huku Panama ikisema hakuna namna yoyote ambapo itayatowa mamlaka yake kwa Marekani. Waziri Mkuu wa Denmark, Mette Frederiksen, amesema kisiwa cha Greenland hakiko kwenye mnada.

Kwa upande wake, Ufaransa imemuonya Donald Trump dhidi ya kile ilichokiita kuwa ni kutishia "mipaka huru" ya Umoja wa Ulaya. Waziri wa Mambo ya nje wa Ufaransa, Jean-Noel Barrot amesema hakuna suala la Umoja wa Ulaya kuruhusu mataifa mengine duniani, au yeyote yule, kushambulia mipaka yake huru.

Hata hivyo Barrot amesema haamini kwamba Marekani itavamia Greenland. Amesema Umoja wa Ulaya  haupaswi kuruhusu kutishwa au kuwa na wasiwasi kupita kiasi, lakini unapaswa kuamka na kujiimarisha.

Hatma ya NATO yaingia matatani ?

Kwa miaka mingi, Marekani na Mexico zinatofautiana juu ya udhibiti wa eneo muhimu la maji ya Mexico yalipo kwenye mpaka kati ya jimbo la Texas na majimbo ya ya Mexico ya Chihuahua, Coahuila, Nuevo Leon na Tamaulipas. Marekani imeliita eneo hilo Rio Grande huku Mexico ikiliita Rio Bravo.

Vitisho hivyo vya Donald Trump vimekuja chini ya wiki mbili kabla ya kuapishwa kwake kama rais wa Marekani. Wachambuzi wanahisi kuwa huenda jumuiya ya kujihami ya NATO ikapitia kipindi kigumu zaidi katika historia yake chini ya muhula huu wa Trump.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW