Kauli ya Kagame yazusha hofu ya usalama kwa raia wa DRC
11 Februari 2022Kagame aliyasema hayo mjini Kigali mwanzoni mwa wiki wakati akiwaapisha mawaziri wapya. Katika matamshi yake Rais wa Rwanda Paul Kagame, alionyesha kwamba kuwepo kwa waasi kinyarwanda wa FDLR pamoja na waganda wa ADF mashariki mwa Kongo kunaendelea kuiweka hatarini nchi yake, na kusisitiza kuwa kuna wakati wa kujadiliana na wakati wa kuamua na kupata suluhisho bila kuomba ruhusa kwa yeyote yule.
Kinachowahuzunisha zaidi wakongomani ni kwamba kamati ya bunge la kitaifa inayohusika na ulinzi na usalama iliwahi kuitolea serikali mapendekezo ili kutatua suala la usalama mashariki mwa nchi hii, lakini hadi sasa hali inaendelea kuzorota katika eneo hilo licha ya kuwekwa utawala wa kijeshi tangu sasa miezi tisa.
Akizungumza na DW, mbunge wa bunge la taifa Gratien de Saint Nicolas Iracan alisema ni muhimu sana kwa waziri mkuu kujieleza bungeni kuhusu jambo hilo.
"Inatupatia woga na ingekuwa vizuri serikali ya Kongo kutueleza namna gani hali ya usalama ilivyo upande wa kwetu. Tuweze kujua serikali inatayarisha kitu gani, tunaogopa kuona leo au kesho jeshi kutoka Rwanda likiingia Kongo kwa sababu hakuna namna ya kulinda usalama. Basi ni vizuri tuweze kujua mambo yanavyoendelea."
Vitisho vya Rais wa Rwanda vimetokea wakati vikosi vya Uganda tayari vipo nchini humu kupambana na waasi kundi la ADF hukohuko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo tangu mwishoni mwa Novemba.
Kuna uwezekano majeshi za Rwanda na Uganda kukutana tena kwenye ardhi ya Kongo, na hii ni moja ya sababu za wasiwasi kwa Wakongomani. Nicoles Kavira, mratibu wa kitaifa wa harakati ya hasira kuhusu usalama wa Kongo, anapinga kabisa mradi wa rais Kagame.
"Tunasikitika sana na ni tunashangaa kuona kiongozi wa nchi nyingine akisema kwamba anataka kuingia tena katika nchi yetu ya Kongo kutafuta adui yake ! Hiyo ni kukanyaga kabisaa maiti ya Wakongomani. Tena tuone walewale majambazi wanatakarudi hapa, hilo tunalikataa kabisaa, tunasema NO."
Baada ya askari wa Rwanda na Uganda kupambana mjini Kisangani mwaka 2000, Wakongomani bado wanayo kumbukumbu mbaya kuhusu maelfu ya watu waliofariki mjini humo pamoja na vitu kadhaa kuharibiwa.