1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nchi za Kiislam zatoa wito wa kususia bidhaa za Ufaransa

26 Oktoba 2020

Baadhi ya nchi za Kiislam zimetoa wito wa kususia bidhaa za Ufaransa ikiwa ni katika kuijibu hatua ya rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron kuunga mkono kitendo cha kuchorwa kibonzo cha Mtume Muhammad.

Frankreich | Paris | Macron bei der Gedenkzeremonie für den Lehrer Samuel Paty 21.10.2020
Picha: Francois Mori/Pool/Reuters

Rais Macron alisema wazi kwamba Ufaransa haitoacha kuchora vibonzo, kutokana na kuchinjwa kwa mwalimu Samuel Paty aliyewaonyesha wanafunzi wake kibonzo cha Mtume Muhammad mapema mwezi huu, katika kitongoji kimoja cha Paris katika somo kuhusu uhuru wa kujieleza. Siku ya Ijumaa vibonzo vya Mtume Muhammad vilichapishwa kwenye majengo ya serikali nchini Ufaransa, hatua iliyoukasirisha ulimengu wa Kiarabu.

Wito wa kususia bidhaa za Ufaransa unavuma kwenye mitandao ya kijamii, huku wananchi wa Misri wakisambaza orodha ya bidhaa za Kifaransa walizoamua kuzisusia. Imam Mkuu wa Chuo cha Kiislamu cha Al-Azhar mjini Cairo, Ahmed al-Tayyeb amesema shambulizi dhidi ya Mtume Muhammad ni sehemu ya kampeni ya kuutumia Uislamu kushinda vita vya kisiasa.

Imam Mkuu wa Chuo cha Kiislamu cha Al-Azhar mjini Cairo, Ahmed al-TayyebPicha: picture-alliance/AP Photo/N. El-Mofty

Nchini Kuwait, mashirika 50 ya ushirikiano wa kibiashara yamesema yameondoa bidhaa zote za Ufaransa katika maduka yake kwenye nchi hiyo ya Ghuba. Aidha, imeripotiwa kuwa maduka ya Qatar pia yameondoa bidhaa za Ufaransa.

Jumuia ya Nchi za Kiislamu, OIC imelaani kitendo cha kuchora vibonzo vinavyomuonesha kiongozi huyo wa dini ya Kiislamu, ikisema ni ''hatari kwa uhusiano'' wa nchi za Kiislamu na Ufaransa. Waziri wa Mambo ya Nje wa Jordan, pia ameikosoa hatua ya Ufaransa iliyotumika kwa kisingizo cha uhuru wa kujieleza.

Wizara ya mambo ya nje ya Morocco imelaani vikali hatua ya kuendelea kuchapishwa vibonzo hivyo, ikisema uhuru wa kujieleza hauwezi kuhalalisha kuitukana dini ya Kiislamu, ambayo ina zaidi ya waumini bilioni mbili ulimwenguni kote.

Ufaransa yajibu

Ufaransa imeukosoa wito wa kususiwa kwa bidhaa zake, ikitaka hatua hiyo ikomeshwe, na kusema kwamba mashambulizi kama hayo ni kazi ya Waislamu wachache wenye itikadi kali na kusisitiza kuhusu msimamo uliotolewa na Rais Macron kwamba Ufaransa haitopiga marufuku uchapishaji wa vibonzo hivyo.

Wakati huo huo, wizara ya mambo ya nje ya Pakistan leo imemuita balozi wa Ufaransa nchini humo kulalamika kuhusu kitendo cha Rais Macron kuunga mkono kuchapishwa vibonzo vya Mtume Muhammad. Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistan, Shah Mehmood Qureshi amesema kuwa matendo kama hayo yanachochea chuki na kuigawa jamii na inaweza kusababisha tatizo kubwa duniani.

Rais wa Uturki, Recep Tayyip Erdogan Picha: Sercan Kucuksahin/AA/picture-alliance

Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan amemtaka Macron ''akapimwe akili'' kutokana na kauli yake hiyo na namna anavyowachukulia mamilioni ya watu kutoka makundi ya imani tofauti.

''Mtu anayeiongoza Ufaransa, Rais Emmanuel Macron amepoteza mwelekeo. Anaendelea kuzungumza kuhusu Erdogan wakati akiwa amelala na akiwa akiwa yuko macho. Nilisema jana nilipokuwa Kayseri, kwamba ana matatizo na kwa kweli anapaswa kupimwa akili,'' alisema Erdogan.

Ufaransa imeijibu kauli hiyo kwa kumuita balozi wake aliyeko Ankara na imeikosoa propaganda ya Uturuki ikisema inalenga kuchochea chuki nyumbani na nje ya nchi.

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Josep Borrell, ameyaita matamshi ya Erdogan kuwa ''yasiyokubalika'' na ameitaka Uturuki kuacha uhasama huo hatari wa kujibizana.

(AFP, DPA, AP, Reuters)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW