Kauli ya Mbappe yaibua hasira China
29 Oktoba 2026
Wakati mashabiki wengi wa soka duniani wakijadili utata ulioibuka kutokana na kauli za nyota wa Real Madrid, Kylian Mbappe, kuhusu aliyekuwa kiongozi wa China Mao Zedong, vita halisi vinaonekana kuhamia kwenye upande wa biashara kuliko mpira wenyewe.
Ndani ya siku mbili tu baada ya video ya Mbappe kusambaa mtandaoni, mshambuliaji huyo, Real Madrid na La Liga walilazimika kuomba radhi kwa haraka kufuatia hasira zilizozuka nchini China. Hata hivyo, wachambuzi wanaamini kuwa changamoto kubwa si kuomba msamaha, bali kurejesha imani ya moja ya masoko makubwa zaidi duniani.
China, yenye zaidi ya watu bilioni 1.4 na uchumi wa pili kwa ukubwa duniani, imekuwa chanzo muhimu cha mapato kwa vilabu vikubwa vya Ulaya kupitia mauzo ya jezi, haki za matangazo na mikataba ya udhamini.
Kauli za Mbappe, ambazo zilionekana kumdharau Mao Zedong kwa kumtaja kama "dikteta wa Kichina" wakati akizungumzia picha iliyohaririwa mtandaoni, na kuibua ghadhabu kubwa miongoni mwa watumiaji mitandao ya kijamii na vyombo vya habari vya serikali nchini humo.
Ingawa wanahistoria wengi humhusisha Mao na vifo vya mamilioni ya watu wakati wa utawala wake, bado anatambuliwa rasmi na serikali ya China kama mwanzilishi wa taifa la kisasa la China na shujaa wa mapinduzi ya Kikomunisti. Hivyo, kumkosoa au kumdharau hadharani ni jambo linalochukuliwa kwa uzito mkubwa.
Athari hazikuchukua muda kuonekana
Baadhi ya chapa kubwa za China ziliripotiwa kusitisha ushirikiano wao wa kibiashara na Mbappe, huku matangazo ya mechi za La Liga yakiondolewa kwenye ratiba za kituo cha televisheni cha taifa, CCTV.
Hatua hiyo imezua wasiwasi mkubwa kwa viongozi wa soka la Uhispania wanaotegemea soko la Asia, hasa China, kuendesha sehemu ya shughuli zao za kibiashara.
Kwa miaka mingi, Real Madrid imejenga ushawishi mkubwa nchini China. Jezi za klabu hiyo zinauzwa kwa idadi kubwa, huku kampuni kadhaa za China zikiwa miongoni mwa wadhamini wake muhimu. Ripoti mbalimbali pia zimekuwa zikionyesha kuwa sehemu kubwa ya mapato ya biashara ya bidhaa za klabu hiyo hutoka katika soko la China.
Hali hiyo ndiyo inayofanya sakata la Mbappe kuonekana kama tishio la moja kwa moja kwa mapato ya klabu na La Liga kwa ujumla.
Mchambuzi wa michezo Yan Qiang anasema kuomba radhi ni muhimu, lakini si tiketi ya kumaliza tatizo moja kwa moja. Anaamini tukio hilo limeathiri kwa kiasi kikubwa taswira ya Real Madrid na La Liga katika moja ya masoko yao muhimu zaidi duniani.
Kwa mujibu wake, katika zama za mitandao ya kijamii, jambo linaweza kuenea kwa kasi na kusababisha hasara kubwa kabla wahusika hawajapata nafasi ya kujitetea. Anaonya kuwa kuomba radhi si lazima kuwe mwisho wa mgogoro huo, hasa ikiwa mashabiki na wadau wa China wataendelea kuhisi kuwa wamepuuzwa au kudharauliwa.
Tukio linajirudia
Historia inaonyesha kuwa China imewahi kuchukua hatua kali dhidi ya mashirika ya michezo yaliyohusishwa na kauli zinazogusa masuala nyeti ya kisiasa.
Mfano maarufu ni ule wa NBA mwaka 2019, baada ya aliyekuwa meneja wa Houston Rockets, Daryl Morey, kuunga mkono waandamanaji wa Hong Kong kupitia mitandao ya kijamii. Mgogoro huo ulisababisha NBA kupoteza mamilioni ya dola kutokana na kusitishwa kwa ushirikiano na vyombo vya habari na wadhamini wa China.
Leo, wachambuzi wanaona sakata la Mbappe likifuata mkondo huo huo.
Swali kubwa linalobaki ni kama msamaha wa Mbappe na taasisi zake utaweza kurejesha imani ya Wachina au kama athari zake zitaendelea kwa miezi au hata miaka ijayo.
Wataalamu wa biashara ya michezo wanaamini kuwa hatua ya kwanza imechukuliwa kupitia kuomba radhi. Hata hivyo, mustakabali wa mahusiano kati ya Mbappe, Real Madrid, La Liga na soko la China utategemea zaidi matendo yao ya baadaye kuliko maneno yao ya sasa.
Kwa sasa, jambo moja linaonekana wazi. Sakata hili limeonyesha kuwa katika ulimwengu wa kisasa wa michezo, kauli moja inaweza kusababisha hasara kubwa zaidi nje ya uwanja kuliko matokeo ya dakika 90 za mchezo.
Na kwa Real Madrid pamoja na La Liga, vita ya kulinda biashara yao nchini China huenda ndiyo mechi ngumu zaidi wanayocheza kwa sasa.