1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kauli ya Trump kuiangamiza Korea Kaskazini yaibua mjadala

20 Septemba 2017

Hisia mchanganyiko zajitokeza kuhusu hotuba ya Trump kuwa Marekani iko tayari kuiangamiza Korea Kaskazini endapo itahitajika. Wapo viongozi wanaosifia kauli hiyo huku wengine wakiikosoa.

UN Generalversammlung in New York | Donald Trump, Präsident USA
Picha: Getty Images/AFP/T.A. Clary

Hotuba ya Rais  Donald Trump wa Marekani katika mkutano wa kila mwaka wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ambapo alisema Marekani ipo tayari kuiangamiza Korea Kaskazini endapo itahitajika kujilinda pamoja na washirika wake, imeendelea kuibua mijadala miongoni mwa viongozi na wachambuzi mbalimbali. Swali likiwa ni je ni kitisho kutokana na sera ambayo Marekani imechukua?

Maafisa na wachambuzi kutoka bara la Asia wamewazia usiku kucha kauli hiyo ya Trump kuwa ataiangamiza kabisa Korea Kaskazini endapo Marekani itachokozwa.

Katika eneo ambalo limezoea vitisho kutokana na juhudi za Korea Kaskazini kutengeneza silaha za nyuklia, kauli ya Trump haikupaswa kuibua mjadala. Lakini imejikuta ikijadiliwa kwa pande zote mbili.

Rais wa Marekani akihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New YorkPicha: Reuters/S. Stapleton

Korea Kusini haikuyakosoa maneno ya Trump huku ikisema ni ishara ya kujitolea kikamilifu kwa Marekani kukabiliana na Korea Kaskazini. Haya ndiyo yalikuwa maneno ya Trump ambaye pia alimuita rais wa Korea Kaskazini kuwa Mtu wa Roketi: "Mtu wa Roketi yuko katika njia ya kujiangamiza mwenyewe na utawala wake. Marekani iko tayari na inao uwezo kuiangamiza kabisa Korea Kaskazini, lakini natumai hiyo haitahitajika."

Lakini Kansela Angela Merkel wa Ujerumani, ambaye hata hivyo hakulitaja jina la Trump, ametoa kauli yake akisema suluhisho pekee kwa mzozo wa nyuklia wa Korea Kaskazini ni diplomasia na kwa njia ya amani.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Javad Zarif, ameikosoa hotuba hiyo akiitaja sio inayotarajiwa katika karne hii ya 21 na haistahili hata kujibiwa. "Kwangu mimi na serikali ya Ujerumani, suluhisho pekee ni njia ya diplomasia ya amani vinginevyo vitasababisha maafa, ninao uhakika. Hivyo ninawaahidi nitafanya kila juhudi kutimiza hilo kwa nguvu zangu zote."

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akitoa hotuba katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New YorkPicha: Reuters/L. Jackson

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameisifia hotuba ya Trump huku akisema kuwa katika miaka thelathini ya tajiriba na Umoja wa Mataifa, hajaona hotuba ya kijasiri na ya waziwazi kama hiyo. Netanyahu ameongeza kuwa "Trump alisema ukweli kuhusu hatari zinazoikumba ulimwengu na akatoa wito imara wa kukabiliana nazo kuhakikisha ubinadamu katika siku zijazo."

Kulingana na msemaji wa rais wa Korea Kusini, Park Soo-hyun, maneno ya Trump yalitilia mkazo haja ya kuwekea Korea Kaskazini vikwazo vya juu zaidi kuhusu mipango yake ya nyuklia na uchokozi kama njia pekee ya kusuluhisha tatizo lililopo.

Lakini wanasiasa wa upinzani nchini Korea kusini wanahofia kuwa maneno ya Trump yanaashiria nchi yao kupoteza sauti na ushawishi wake kimataifa katika juhudi za kukabiliana na mipango ya nyuklia ya Korea Kaskazini.

Japan, kwa upande wake, ilitilia maanani Trump alipotaja raia wa Japan wanaoshikiliwa na Korea Kaskazini. Wachambuzi kutoka Asia walishangazwa na kuingiwa hofu kuwa maneno ya Trump yaliakisi vitisho ambavyo hujitokeza kupitia shirika la habari linalomililkiwa na serikali ya Korea Kaskazini.

Mkutano huo unaingia siku yake ya pili leo Jumatano.

Mwandishi: John Juma/APE/AFPE

Mhariri: Mohammed Khelef

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW