Kauli za Rais Samia zazusha mjadala kuhusu haki za binaadamu
25 Novemba 2022Pamoja na mambo mengine, Rais Samia amesema atatumia sheria za nchi kuwabana wanaharakati wanaomkosoa na kuwaita kuwa ni maadui wa serikali yake.
Akiwa jijini Arusha kaskazini mwa Tanzania wakati wa ufunguzi wa mkutano wa 27 wa Jumuiya ya Wanasheria wa Afrika Mashariki jana, pamoja na mambo mengine, Rais Samia alionesha kuchukizwa na utendaji kazi uliopitiliza wa Chama cha Wanasheria Tanganyika, TLS, akisema kwamba hakikuwa chama kinachosimamia utawala wa sheria bali ni chama cha wanaharakati waliokuwa wanaikosoa serikali, akitishia kwamba katika utawala wake hawezi kushirikiana na watu wanaomkosoa aliowaita maadui.
Nchi za Afrika zatakiwa kulinda haki za binaadamu
Kauli hiyo imepokelewa kwa namna tofauti na wachambuzi wa masuala ya kisiasa pamoja na wanasheria, huku wengi wakisema kuwa wanasheria wa Tanzania kupitia chama chao cha TLS wanao wajibu kulingana na katiba ya Tanzania ya kutetea haki za binaadamu, kulinda utawala wa kisheria na kuikosoa serikali inapokwenda kinyume cha sheria na kuvunja haki hizo na sio kweli kwamba kukosoa watawala na viongozi wa serikali ni kwenda kinyume cha sheria.
Katika hotuba yake pia, Rais Samia hakuweka bayana kama nchi yake itajiunga tena katika Itifaki ya Mahakama ya Afrika ya Haki za Binaadamu na Watu iliyopo Arusha, Tanzania, ili kuruhusu raia wake na mashirika binafsi kupeleka kesi zinazohusu haki za binaadamu, baada ya kujiondoa katika itifaki hiyo wakati wa utawala wa Hayati Rais John Magufuli.
Mashirika ya haki za binadamu yatoa wito wa majadiliano Tanzania
Kujiondoa kwa Tanzania katika itifaki hiyo ya mahakama ya Afrika ni kitendo kinachotafsiriwa kama kuondoa ulinzi wa masuala ya haki za binaadamu kwa raia na hivyo na matarajio ya Watanzania ni nchi hiyo kujizatiti na kuwajibika kulinda haki za binaadamu na utawala wa kisheria.