1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Kaulimbiu ya "ikomboe Hong Kong" yamulikwa katika kesi nyeti

Josephat Charo
26 Julai 2021

Majaji watatu wa Hong Kong wataamua Jumanne ikiwa kauli mbiu ya maandamano ya "Ikomboe Hong Hong, Mapinduzi ya nyakati zetu, ni wito wa kutaka kujitenga, katika hukumu yao ya kesi dhidi ya mtumishi mmoja wa mgahawani.

Hongkong | Messerangriff auf Polizisten
Picha: Miyuki Yoshioka/The Yomiuri Shimbun/AP/picture alliance

Wataalamu wa sheria wanasema hukumu hiyo ya kihistoria huenda ikawa na athari za muda mrefu kwa jinsi sheria ya kitaifa ya usalama iliyowekwa na China katika mji wake wenye uhuru mkubwa kabisa mwaka mmoja uliopita dhidi ya ugaidi, na kushirikiana na nchi za kigeni, itakavyobadilisha sheria zake za kitamaduni.

Wanaharakati kwa upande wao wanasema hukumu ya kufuta kauli mbiu hiyo itazidi kukaba koo uhuru wa kutoa maoni na kujieleza.

Kauli mbiu hiyo ilitumika sana wakati wa maandamano ya kuunga mkono demokrasia, ikachapishwa kwenye mtandao, ikachorwa kwenye kuta na kuchapishwa kwenye vijitabu, vipeperushi, vibandiko na fulana, mpaka vikombe vya kunywea chai.

Soma pia: Amnesty: Sheria ya usalama wa kitaifa imeangamiza uhuru Hong Kong

Wakati wa siku 15 za kusikilizwa kwa kesi hiyo dhidi ya Tong Ying-lit, muhudumu kwenye mgahawa, korti ilifahamishwa jinsi alivyoendesha pikipiki yake akiwa amebeba  bendera nyeusi iliyokuwa na maneno ya kauli mbiu hiyo na kuwagonga maafisa wa polisi wa kupambana na fujo katikati mwa Hong Kong mnamo Julai mosi mwaka uliopita.

Baadhi ya watetezi wa haki za binadamu waliokamatwa Hong Kong.Picha: Isaac Lawrence/AFP/Getty Images

Tong alikuwa mtu wa kwanza kushitakiwa chini ya sheria mpya ya kitaifa ya usalama.

Mwendesha mashitaka mkuu wa serikali Anthony Chau alijenga hoja mahakamani kwamba hiki kilikuwa kitendo cha kigaidi na Tong alitaka kuwachochea watu wadai uhuru wa Hong Kong kutoka kwa China bara, makosa mawili makubwa chini ya sheria mpya ya usalama ambayo yanaweza kumfanya kuhukumiwa kifungo cha miaka kadhaa gerezani, iwapo atatiwa hatiani.

Soma pia: China yamulikwa kwa ukiukaji wa haki za binaadamu

Tong amekanusha kuwa na hatia katika mashitaka ya ugaidi, uchochezi wa kufanya watu wajitenge na uendeshaji hatari wa pikipiki ambao ulisababisha majeraha mabaya ya kimwili. Chau hakujibu maombi ya kutoa kauli kuhusiana na kesi hii na wakili anayemtetea Tong, Clive Grossman, pia alikataa kusema lolote.

Kiini cha kesi hiyo kimekuwa hoja ya mwendesha mashitaka kwamba kauli mbiu hiyo inazungumzia uhuru wa Hong Kong, msimamo ambao haukubaliki kabisa na China, ambayo inakiona kisiwa cha Hong Kong ambacho zamani kilikuwa koloni la Uingereza, kama sehemu ya himaya yake.

Mjadala kuhusu maana ya kaulimbiu hiyo

Wakati wa kusikilizwa kwa kesi dhidi ya Tong, maana ya kauli mbiu hiyo ilijadiliwa sana kwa kina katika malumbano yaliyoibua kumbukumbu za wafalme wa China, mwandishi wa mashairi wa zamani wa China Li Bai, Malcolm X, viongozi katili wa Mongolia na kiongozi wa zamani wa kizalendo wa China, Chiang Kai-shek.

Mhariri mtendaji wa gazeti la Apple Daily akitoa ishara katika makao makuu ya gazeti hilo mjini Hong Kong, Juni 23, 2021, kabla ya gazeti hilo kusitisha uchapishaji siku iliyofuata kutokana na shinikizo la utawala wa China.Picha: Kin Cheung/AP/picture alliance

Upande wa waendesha mashitaka uliiambia mahakama kwamba kauli mbiu hiyo ilianzishwa mwaka 2016 na mwanaharakati wa Hong Kong, Edward Leung, wakili maarufu anayetetea uhuru wa Hong Kong. Leung anatumikia kifungo cha miaka sita jela kwa kufanya mgomo na hakupatikana kutoa kauli. Hakukutolewa kauli ya moja kwa moja na mawakili wawili waliomtetea.

Soma pia: Maoni: China yakomesha utawala wa demokrasia Hong Kong

Mtaalamu shahidi wa upande wa waendesha mashitaka, profesa wa historia Lau Chi.pang, alishuhudia kwamba sehemu ya kwanza ya kauli mbiu hiyo ya kichina imetumiwa katika historia ya China kutoka Qin hadi falme za Qing, na kwamba maana ya kuikomboa himaya iliyopotea au kumfukuza adui haijabadilika katika kipindi cha miaka elfu moja. Lau aliiambia mahakama maneno ya kauli mbiu hiyo yana maana moja tu: yanahusu kuitenganisha Hong Kong kutoka kwa utawala wa Jamhuri ya Umma wa China.

Katika kauli yake ya kufunga hoja Jumanne iliyopita, wakili anayemtetea Tong, Grossman, alisema waandamanaji ulimwenguni kote mara kwa mara hubeba mabango bila kukabiliwa na mashitaka na kwamba Tong anatakiwa aachiwe huru ikiwa maana ya kauli mbiu hiyo haiwezi kufafanuliwa moja kwa moja.

Chanzo: Mashirika

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW