1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Kazakhstan: Zaidi ya 160 wauawa, 5,000 wakamatwa

10 Januari 2022

Zaidi ya watu 160 wameuawa na karibu 8,000 wamekamatwa katika vurugu zilizoitikisa Kazakhstan wiki iliyopita, huku rais wa taifa hilo Kassym-Jomart Tokayev akisema machafuko hayo yalikuwa jaribio la mapinduzi.

Kazachstan | Proteste in Almaty - Sicherheitskräfte
Picha: Vladimir Tretyakov/AP/picture alliance

Shirika la habari la Sputnik la nchini Urusi limeinukuu wizara ya afya ya Kazakhstan ikisema kuwa jumla ya watu 164, wakiwemo watoto wawili, waliuawa katika vurugu mbaya zaidi kuwahi kushuhudiwa katika miaka 30 ya uhuru wa taifa hilo.

Imesema watu 103 walikufa katika mji mkuu wa Almaty, ambako machafuko mabaya zaidi yalitokea.

Siku ya Jumapili, kulishuhudiwa utulivu kiasi katika mji huo ambao ndiyo kitovu cha uchumi wa Kazakhstan, ambapo polisi ilikuwa ikifyatua risasi hewani kuzuwia watu kusogelea bustani kuu ya mji.

Winchi likipakia lori la jeshi lililochomwa wakati wa makabiliano mjini Almaty, Jumapili Januari 9, 2022.Picha: Vladimir Tretyakov/NUR.KZ/AP/picture alliance

Kwa ujumla, watu 7,939 wamekamatwa kwa ajili ya kuhojiwa, kama sehemu ya chunguzi 125 tofauti juu ya machafuko hayo, imesema wizara ya mambo ya ndani.

Soma pia: Watu 164 wameuwawa, machafuko ya Kazakhstan

Mzozo huo ulichochewa wiki iliyopita katika maeneo ya mkoa wa magharibi na kuogezeka kwa bei za mafuta, lakini kwa haraka sana ukaifikia miji mikubwa, ikiwemo Almaty, ambako fujo zilizuka.

Katika kujibu vurugu hizo, rais Kassym-Jomart Tokayev alitoa amri ya kuua ili kuzima machafuko hayo ambayo ameyalaumu kwa kile alichokiita majambazi na magaidi.

"Kundi la wanamgambo wenye silaha waliokuwa wanasubiri fursa walijiunga na maandamano. Lengo kuu likawa wazi: kudhoofisha utaratibu wa kikatiba, uharibifu wa taasisi za serikali, utwaaji wa madaraka," alisema rais Tokayec. "Tunazungumzia jaribio la mapinduzi."

Uingiliaji wa muungano wa usalama wa CSTO

Kwa mwaliko wa Tokayev, muungano wa kijeshi unaoongozwa na Urusi wa Shirika la Mkataba wa Pamoja wa Usalama CSTO, ulituma majeshi kurejesha amani, uingiliaji ambao umekuja wakati kukiwa na mzozo mkubwa katika uhusiano kati ya Urusi na Marekani, kuelekea mazungumzo juu ya mzozo wa Ukraine.

Rais wa Urusi Vladmir Putin akizungumza na wakuu wa mataifa ya shirika la CSTO kuhusu hali nchini Kazakhstan, Januari 10, 2022.Picha: Aleksey Nikolskyi/Kremlin/Sputnik/REUTERS

Rais wa Urusi Vladmir Putin, amesema katika mkutano wa viongozi wakuu wa mataifa ya muungano wa CSTO, unaofanyika kwa njia ya video kutokea Moscow, kwamba vikosi vya Urusi vilivyopelekwa Kazakhstan vitakuwepo kwa muda tu.

Soma pia: Tokayaev apuuza mazungumzo na waandamanaji Kazakhstan

Mbali na Urusi na Kazakhstan, mataifa ya Armenia, Belarus, Kyrgyzstan na Tajisktan pia ni wanachama wa muungano huo.

Kiongozi wa zamani wa Kazakhstan, Nursultan Nazarbayev ndiye alikuwa mtawala wa muda mrefu zaidi wa taifa hilo hadi alipokabidhi madaraka ya urais kwa Tokayev mwaka 2019.

Familia yake hata hivyo inaendelea kuwa na ushawishi mkubwa mjini Nur-Sultan, ambao ndiyo mji mkuu unaobeba jina lake.

Siku ya Jumatano, Tokayev alimuondoa Nazarbayev katika nafasi ya mkuu wa baraza la usalama la taifa, wadhifa ambamo aliendelea kuwa na ushawishi mkubwa.

Chanzo: Mashirika

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW