Kazi ya kujumlisha kura zasimama kwa muda Kwale
10 Agosti 2022Makaratasi hayo yamepatikana yakiwa yamefungiwa ndani ya debe moja. Dosari hiyo hata hivyo inasemekana itachelewesha shughuli ya kujumlishwa kura katika kaunti ya Kwale Hiki ni kituo cha kujumlisha kura cha Babla ambapo kura kutoka vituo mia moja hamsini na nne kutoka eneo bunge la Msambweni zilizohesabiwa zinajumlishwa.
Zoezi hili hata hivyo limesimama kwa muda kufuatia kukosekana kwa baadhi ya karatasi muhimu zilizokuwa zinahitajika katika zoezi la kujumlisha kura. Maafisa wa usalama wameweka ulinzi mkali kuhakikisha kuwa zoezi hili linakamilika bila tashwishi yoyote. Wananchi wa kwale nao walikita kambi nje ya kituo hicho wakisubiri matokeo ya viongozi wao.
Taarifa ya kuchelewa kutangazwa matokeo
Kulingana na Msimamizi wa kituo hiki cha Babla Omara Japheth,wamesuluhisha hilo lakini watachelewa kutangaza matokeo baada ya kukamilisha ujumlishaji wa kura zilizowasilishwa hapa. Aidha Mapema leo Kumekuwa na utata katika kituo hiki baada ya madebe haya ya kura kutoka kituo cha kupigia kura cha mwakigwena kuwasilishwa kituoni yakiwa yamefungwa na kibanio kimoja kinyume na maagizo ya tume huru ya uchaguzi IEBC
Madebe haya yamezuiliwa kwa muda na maafisa waliokuwa hapa na kufanyiwa uchunguzi kabla kuongezwa kwenye orodha ya yale yanayojumuishwa.Katika kaunti ya kwale kumekuwa na kinyang'anyiro kikali baina ya naibu wa gavana Fatuma Achani wa mrengo wa UDA na Profesa Hamadi Boga wa chama cha ODM. Na kufikia sasa Hamadi Boga anaongoza kwa kura za kutoka baadhi ya vituo vya maeneo bunge ya kaunti ya kwale.
Soma zaidi:Ruto na Odinga jino kwa jino Kenya
Kura bado zinahesabiwa katika maeneo mengine ya kaunti ya Kwale na mshindi atajulikana hapo Kesho.
DW: Kwale