1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUingereza

Keir Starmer achukua wadhifa wa Waziri Mkuu wa Uingereza

5 Julai 2024

Kiongozi wa chama cha Labour cha Uingereza Keir Starmer amechukua wadhifa wa Waziri Mkuu leo baada ya chama chake kupata ushindi wa kishindo katika uchaguzi mkuu uliofanyika jana Alhamisi.

Waziri Mkuu mpya wa Uingereza Keir Starmer
Waziri Mkuu mpya wa Uingereza Keir Starmer Picha: Kin Cheung/AP Photo/picture alliance

Ushindi huo unahitimisha enzi ya serikali ya chama cha kihafidhina cha Conservative, kilichokaa madarakani kwa miaka 14. 

Starmer amechukua wadhifa huo muda mfupi baada ya kukutana na Mfalme Charles III kwenye la Buckingham na kuombwa rasmi kuunda serikali mpya. Mwanasiasa huyo amekiongoza chama chake kupata ushindi mkubwa kabisa na wa kihistoria katika uchaguzi wa hapo jana.

Anachukua nafasi ya Rishi Sunak ambaye amelazimika kuachia ngazi baada ya chama chake cha Kihadhina, Conservatives kupata matokeo mabaya zaidi kuwahi kushuhudiwa katika historia ya zaidi ya karne mbili tangu kuundwa kwa chama hicho.

Chama cha Labour kimejizolea zaidi ya viti 400 vya bunge, idadi inayokipa udhibiti kamili wa baraza hilo la kutunga sheria kitu ambacho ni nadra kutokea katika siasa za nchi hiyo.

Matokeo hayo ni pigo lisilo mfano kwa Wahafidhina ambao wameambulia idadi ya kiasi viti 130 pekee wakipoteza zaidi ya majimbo 210 ya uchaguzi. Waziri Mkuu wa zamani Liz Truss ni miongoni mwa wabunge wa Conservative waliokataliwa na wapiga kura.

Sunak atoa hotuba ya kuaga na kuwasilisha barua ya kujiuzulu 

Rishi Sunak akitoa hotuba ya mwisho kabla ya kuachia wadhifa wa Waziri Mkuu wa Uingereza.Picha: Henry Nicholls/AFP/Getty Images

Muda mfupi uliopita Waziri Mkuu anayeondoka madarakani Rishi Sunak alitoa hotuba ya kuaga mbele ya lango la kuingia ofisi na maakazi ya kiongozi wa nchi hiyo yaliyopo mtaa wa Downing katika mwa mji mkuu, London.

Ameisifu rikodi yake ya kiasi miezi 20 ya kuwa waziri mkuu lakini pia akatangaza kwamba ataachia ngazi ya uongozi wa chama cha Conservative.

"Kufuatia matokeo haya nitajiuzulu wadhifa wangu wa uongozi wa chama, siyo mara moja, lakini baada ya kuwepo utaratibu mzuri wa kumpata mrithi wangu. Ni muhimu baada ya miaka 14 chama cha Conservative kijijenge upya na muhimu zaidi kijiandae kuchukua jukumu lake la upinzani kwa ustadi na viwango." amesema Sunak muda mfupi kabla ya kuondoka kwa mara ya mwisho kwenye ofisi ya waziri mkuu.

Alipozungumza hapo baada ya matokeo kuonesha chama chake kimepata pigo, Sunak alisema umma wa Uingereza umetoa hukumu ya kufadhaisha na kwamba anabeba dhima yote ya fedheha iliyowapata Wahafidhina.

Starmer asifu mageuzi ndani ya Labour kuwa sababu ya ushindi 

Kwa upande wake Starmer alitumia hotuba yake ya ushindi kuwasifu Waingereza kwa uamuzi waliochukua na kuahidi kuwatumikia kwa moyo wote kutimiza ahadi za kampeni. Ama kuhusu ushindi wa mserereko ambao chama chake umepata Starmer amesema.

Ofisi za Waziri Mkuu wa Uingereza kwenye mtaa wa Downing mjini London.Picha: Frank Augstein/dpa/AP/picture alliance

"Asubuhi hii tumeshuhudia umma wa Uingereza ukiamua kufunua ukurasa mpya baada ya miaka 14. Ushindi wa uchaguzi haushuki kutoka mbinguni, (bali) unatokana na mapambano na huu wa leo unatokana na mabadiliko ndani ya chama cha Labour. Tumepata nafasi ya kuja kufanya mageuzi kwenye kila sekta kwa sababu tumekifanyia mageuzi chama hiki." amesema Starmer.

Starmer anaingia madarakani akiwa na kibarua kigumu cha kutimiza ahadi za wakati wa kampeni za kuunusuru uchumi wa Uingereza uliokuwa kwenye hali mbaya miaka ya karibuni, kuimarisha huduma za jamii na kurejesha imani ya wapigakura kwa wanasiasa baada ya miaka miwili ya patashika zilizojumuisha tabia za uongo na ulaghai hasa wakati Boris Johnson alipokuwa waziri mkuu.

Salamu za pongezi zamiminika kufuatia ushindi wa Labour 

Kufuatia ushindi wa Labour na Starmer kuwa waziri mkuu salamu za pongezi zinamiminika kutoka kila pembe ya dunia.

Rais Emmanuel Macron wa UfaransaPicha: Aurelien Morissard/AP Pool/dpa/picture alliance

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa amesema nchi yake inatarajia kuendelea kufanya kazi na Uingereza na kwamba anatumai kupata ushirikiano kutoka kwenye serikali mpya.

Waziri Mkuu wa India Narendra Modi amemsifu Starmer kwa ushindi wa kishindo lakini pia amemshukuru Sunak kwa kuimarisha mahusiano na India.

Salamu nyingine za pongezi zimetolewa na marais wa Halmashauri Kuu na Baraza Kuu la Umoja wa Ulaya, viongozi wa Australia, Norway, Ukraine, Israel, Ugiriki na hata China.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW