Keita ashinda uchaguzi Mali
14 Agosti 2013Ni jambo ambalo si kawaida kutokea baada ya uchaguzi, hasa katika nchi za Kiafrika. Jumatatu jioni, mgombea wa urais Soumaila Cissé, alikwenda nyumbani kwa mpinzani wake Ibrahim Boubacar Keita na kumwambia kuwa amekubali kushindwa. Cissé alimpongeza mwenzake akisema: "Wewe ni kaka yangu, na ni jukumu langu kukupongeza kama mkubwa wangu kwa ushindi wako."
Akijibu kauli hiyo ya Cissé, Keita alimwambia kupitia televisheni ya Mali "Umefanya hili si kwa ajili yako tu, bali kwa maslahi ya Mali. Ziara yako ni alama kwa Mali mpya."
Ingawa matokeo rasmi bado hayajatolewa, Cissé anafahamu kuwa hawezi kushinda uchaguzi. Tangu awali ilikuwa wazi kwamba Keita atapata kura nyingi zaidi. Raia wa Mali walifurahishwa na jambo hilo, kama anavyosema mkaazi mmoja wa mji mkuu, Bamako: "Ninawapongeza wananchi wa Mali kwa sababu wao ndio walioshinda. Kwa kifupi, wao ndio washindi wa uchaguzi huu."
Waangalizi wameridhika
Waangalizi wa kimataifa nao wamependezwa na namna uchaguzi huu ulivyoendeshwa, wakisema kuwa ulikuwa wa wazi na wa haki. Katika duru ya pili inakadiriwa kwamba asilimia 45 tu ya watu wenye haki ya kupiga kura walifika katika vituo vya kupiga kura. Louis Michel ni mkuu wa ujumbe wa waangalizi kutoka Umoja wa Ulaya: "Waangalizi wa Umoja wa Ulaya wamefanya tathmini ya uchaguzi na kuona kwamba mambo yalikwenda sawa katika asilimia 99 ya vituo 831 vya kupigia kura walivyovitembelea," alisema.
Sasa rais mteule Keita atakuwa na muda wa siku 60 kuunda serikali na kuanzisha mazungumzo ya kuleta amani ya kudumu katika maeneo mengi.
Hii ni mara ya tatu kwa Keita kugombea urais. Alijaribu mwaka 2002 na 2007 na kushindwa mara zote. Hivi sasa anakabiliwa na changamoto nyingi. Ibrahima Sangho wa shirika la usimamizi wa uchaguzi Mali, APEM anaeleza kuwa hakuna mwanasiasa atakayeweza kuiendesha Mali kwa namna ilivyokuwa ikiendeshwa katika miaka 20 iliyopita. "Wananchi watamwangalia rais mpya kwa makini na kufuatilia kama atatekeleza ahadi alizotoa wakati wa kampeni. Ahadi ya kwamba wananchi wataweza kuishi kwa amani na utulivu." Katika kampeni zake Keita aliahidi kurejesha heshima ya nchi yake iliyoingia katika machafuko, hasa katika eneo la kaskazini.
Mwandishi: Elizabeth Shoo/ap/dpa
Mhariri: Mohammed Khelef