Keita ashinda uchaguzi Mali
16 Agosti 2018Kwa mujibu wa matokeo rasmi yaliyotangazwa leo na wizara ya utawala wa ndani, Keita mwenye umri wa miaka 67 amepata asilimia 67.17 ya kura zilizopigwa Jumapili iliyopita, huku mpinzani wake, Cisse akiwa amepata asilimia 32.83. Asilimia 34.5 ya watu ndiyo walijitokeza kupiga kura. Cisse, mwenye umri wa miaka 68 na waziri wa zamani wa fedha pia aligombea urais dhidi ya Keita mwaka 2013.
Chama cha Cisse kimeapa kuyapinga matokeo hayo kwa kutumia njia za kidemokrasia. Siku ya Jumatatu, Cisse alitangaza kwamba atayapinga matokeo na kuwataka wananchi wa Mali kusimama pamoja kupinga udikteta wa udanganyifu, kauli ambayo iliusababisha Umoja wa Mataifa kutoa wito wa kuwepo utulivu.
Keita ni mgombea wa watu
Akizungumza baada ya matokeo kutangazwa, meneja wa kampeni wa Rais Keita, Bacary Treta amesema kamwe hawajawahi kufanya makosa kumsimamisha Keita.
''Katika duru ya kwanza Keita alishinda kwenye mikoa yote ya Mali, nje na ndani ya wilaya ya Bamako. Hivyo mnaweza mkajionea wenyewe kuwa Keita aliwashinda tangu mwanzo wagombea wote. Siku zote tumekuwa tukisema Keita ndiye mgombea wa watu wa Mali,'' alisema Bacary.
Wakati wafuasi wa Keita wakishangilia ushindi, kiongozi wa kampeni wa Cisse, Tiebile Drame ameyapuuza matokeo hayo akisema ni ya uongo. Drame amesema Cisse anapanga kukata rufaa katika Mahakama ya Katiba ili kuyafuta baadhi ya matokeo yaliyo na udanganyifu kwenye mikoa kadhaa.
Waangalizi wa uchaguzi wa Umoja wa Ulaya na Umoja wa Afrika awali walitoa ripoti, wakisema uchaguzi huo haukuwa mbaya sana. Mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Ulaya, Cecile Kyenge amesema waangalizi wao hawakuona udanganyifu, ingawa kulikuwa na kasoro. Umoja wa Afrika kwa upande wake umesema kura zilipigwa katika mazingira yanayokubalika.
Uchaguzi uligubikwa na machafuko
Hata hivyo, uchaguzi huo uligubikwa na mashambulizi yaliyofanywa na wapiganaji wa jihadi, hatua iliyolazimu kufungwa kwa vituo vya kupigia kura vyenye watu wachache. Wagombea watatu wakuu wa upinzani waliyapinga matokeo ya duru ya kwanza, wakisema uchaguzi uligubikwa na udanganyifu, lakini ombi lao lilikataliwa na Mahakama ya Katiba.
Keita ataapishwa rasmi Septemba 4, kuiongoza Mali kwa kipindi cha miaka mitano huku akiwa anakabiliwa na kibarua kizito cha kuyaimarisha makubaliano ya amani ya mwaka 2015 yaliyofikiwa kati ya serikali, makundi yanayoiunga mkono serikali na waasi wa zamani wa Tuareg.
Pia ana jukumu kubwa la kuiondoa Mali katika wimbi la machafuko ya makundi ya itikadi kali na kikabila katika eneo la kati na kaskazini mwa nchi ambako mashambulizi yaliongezeka katika miezi ya kabla ya uchaguzi, licha ya kuwepo kwa majeshi ya Umoja wa Mataifa na Ufaransa.
Changamoto nyingine kwa Keita ni kuuimarisha uchumi katika nchi hiyo ambayo karibu nusu ya watu milioni 18 wanaishi katika umasikini.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFP, Reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman