1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya: Abiria 239 toka China watakiwa kujiweka karantini

Thelma Mwadzaya27 Februari 2020

Serikali ya Kenya imejikuta pabaya baada ya abiria 239 kwenye ndege iliyotokea China kutua na kuruhusiwa kuingia nchini saa chache zilizopita

Coronavirus
Picha: picture-alliance/AP/NIAID-RML

 Abiria hao waliagizwa kujiweka kwenye karantini kwa muda wa siku 14 kama njia ya kuuondoa uwezekano wa virusi vya Corona kusambaa iwapo wameambukizwa.

Ndege hiyo ya kampuni ya China South iliwasili kwenye uwanja wa kimataifa wa JKIA na nusura abiria wake wanyimwe idhini ya kuingia nchini humo kwasababu ya kuhofia virusi vya Corona kusambaa. Haya yanajiri wakati ambapo safari za kutokea na kuelekea China kwa ndege zilipigwa marufuku wiki kadhaa zilizopita. Hofu imetanda kuwa huenda yupo aliyeambukizwa homa hiyo hatari jambo linalozua wasiwasi.

Hata hivyo kwenye taarifa yake msemaji wa serikali alishikilia kuwa hakuna haja ya kuwa na hofu kwani tahadhari zote zinachukuliwa.Taarifa yake ilisisitiza kuwa hakuna anayeruhusiwa kupandandege na kutua JKIA kabla ya kupimwa na kukaguliwa inavyostahili. Muda mfupi uliopita, akiwa mbele ya bunge,Waziri wa mambo ya kigeni Raychelle Omamo amesisitiza kuwa Kenya imejihami.

Hata hivyo tukio hilo limewaacha wengi na maswali kwani msimamo wa serikali ya Kenya umekuwa kwamba raia wake walionasa mjini Wuhan ilikoanzia homa ya corona hawatarejeshwa nyumbani kwani wako salama waliko nchini China. Familia za watu 91 walioko Wuhan zimekuwa zikiirai serikali kuwasaidia jamaa zao warejeshwe bila mafanikio. Wakenya hao tayari wameshatumiwa hela ya matumizi ya kila siku na serikali kuu. Ifahamike kuwa China yenyewe imepiga marufuku safari zozote kutokea eneo uliko mji huo wa Wuhan.

Yote hayo yakiendelea, watu wawili waliopimwa mwishoni mwa juma lililopita huko Kisumu na Bomet hawakukutwa na virusi vya corona. Wawili hao walikuwa wamesafiri kutokea China hivi karibuni. Kufikia sasa watu 15 waliopimwa nchini Kenya hawajapatikana na maambukizi ya homa hiyo hatari ya Corona.

Kwa upande mwengine,kampuni ya ndege ya Kenya iliyositisha safari zake za Nairobi hadi China imeweka bayana kuwa inakabiliwa na hasara kubwa. Mwanzoni mwa wiki hii kampuni hiyo ilitangaza kuwa imepoteza pato la shilingi milioni 800 tangu marufuku hiyo kuendelea kutekelezwa. Alan Kilavuka ni afisa mkuu mtendaji wa kampuni ya ndege ya Kenya na anasisitiza kuwa wanachukua tahadhari zote.

Hata hivyo kampuni ya ndege Ethiopia bado inasafirisha abiria hadi Nairobi kutokea Guangzou kupita Addis Ababa. Kampuni ya ndege ya China Eastern ina safari 3 kwa wiki kutokea Guangzou kupitia Bangkok hadi Nairobi. Kampuni ya ndege ya Kenya bado inaendelea na safari zake za kutokea Nairobi hadi Bangkok. Shirika la Afya Ulimwenguni WHO limetahadharisha kuwa Kenya ni moja ya mataifa ambayo huenda yakaathiriwa na virusi vya Corona kwasababu ya uhusiano wake wa kibiashara na China.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW