1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya bado yatafakari kupeleka askari nchini Haiti

12 Machi 2024

Hali inazidi kuwa mbaya nchini Haiti na magenge ya kihalifu yameudhibiti mji mkuu Porta-Au-Prince,Kenya lakini inataka kupeleka kikosi chake cha askari kuongoza ujumbe wa kimataifa wa kuweka amani Haiti.

Polisi wa kukabiliana na fujo wakiwa Kibera Kenya
Kikosi cha Polisi wa kukabiliana na fujo wa KenyaPicha: Brian Inganga/AP Photo/picture alliance

Kenya imesema kikosi chake cha polisi hivi karibuni kitakwenda nchini Haiti kukabiliana na magenge yanayoendesha hujuma na kuudhibiti mji mkuu,Porta-Au-Prince. Hata hivyo ongezeko la ukosefu wa usalama na hali ya kutokuwepo uhakika inayozunguka suala la ufadhili wa kikosi hicho, ni mambo yanayosababisha mashaka kuhusu uwezekano wa ujumbe huo kwenda Haiti.

Serikali ya Kenya ambayo mwanzoni iliahidi kuongoza ujumbe wa kimataifa wa kikosi cha kulinda usalama mnamo mwezi Julai, inasema sasa kikosi chake kiko tayari kwenda nchini humo baada ya kusaini makubaliano na serikali ya Haiti tarehe mosi mwezi huu wa March.

Mkataba huo ulidhamiriwa kuupatia majibu wasiwasi uliokuwepo, ulioibuliwa na jaji nchini Kenya aliyesema kwamba mpango wa kupeleka kikosi cha polisi cha Kenya nchini Haiti unakwenda kinyume cha sheria.

Nchi zenye nguvu zaishinikiza Kenya

Hatua ya Marekani na mataifa mengine yenye nguvu ya kushinikiza kikosi cha maafisa polisi kutoka Kenya kipelekwe Haiti inaonekana kama hatua ya mwanzo ya kutaka kufungua njia kwa nchi nyingine za Afrika na Carribean nazo pia kupeleka vikosi vyao vya usalama.

Waziri mkuu Ariel Henry ambaye alishindwa kurejea nyumbani Haiti kutokana na kusambaa kwa machafuko tangu aliposaini makubaliano na Kenya, sasa ameshatangaza kujiuzulu. Amesema ataachia ngazi pindi baraza la mpito na kiongozi wa muda atakapoteuliwa.

Polisi wa Kenya wakiyakabili maandamano ya kuipinga serikali Julai 2023Picha: THOMAS MUKOYA/REUTERS

Hali ya kikosi cha askari wa Kenya

Maafisa wa polisi wa Kenya hawajawahi kupelekwa kulinda usalama kwa idadi kubwa kama hii inayotakiwa kwenda Haiti. Na ndani ya nchi hiyo ya Afrika Mashariki kuna masuala tete ambayo bado hayajapatiwa ufumbuzi. Jeshi la Kenya hata hivyo limewahi kupelekwa huko nyuma katika mataifa kadhaa ikiwemo Somalia.Soma pia.Waziri Mkuu wa Haiti kuondoka Ijumaa

Murithi Mutiga ambaye ni mkurugenzi wa mipango inayohusu Afrika katika shirika la kimataifa linaloshughulikia migogoro anasema hali ya usalama inayodorora inaweza ikailazimisha serikali mjini Nairobi kutafakari upya. Mtaalamu huyo anasema serikali inaonesha imegawika na hali ya usalama imezidi kuwa mbaya kuliko wakati Kenya ilipojitolea kuongoza kikosi hicho cha usalama cha kimataifa. Sio Ofisi ya rais wala serikali,wote hawakujibu walipoombwa kutowa tamko.

Changamoto

Moja ya changamoto kubwa kwa mujibu wa wanadiplomasia wanaofahamu kinachoendelea kuhusu suala hili, ni ufadhili. Marekani inatowa kiwango kikubwa cha fedha kwaajili ya ujumbe huo ambao umeshapata ridhaa ya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa tangu mwezi Oktoba mwaka jana.Soma pia:Machafuko mabaya yaikumba Haiti

Kiongozi wa magenge HaitiPicha: REUTERS

Marekani imeahidi kutowa dola milioni 300. Hata hivyo kwa mujibu wa msemaji wa Umoja wa Mataifa, kufikia siku ya Jumatatu ni chini ya dola milioni 11 ambazo zimetolewa na kuwekwa katika mfuko maalum ulioundwa wa Umoja wa Mataifa. Afisa mmoja mwandamizi katika wizara ya mambo ya nje ya Marekani amesema serikali ya rais Joe Biden inafanya kazi na bunge kujaribu kutolewa fedha zilizobakia.

Kenya inataka ilipwe gharama za kupeleka askari wake Haiti lakini sheria za Umoja wa Mataifa zinahitaji fedha zinazotolewa zitumike tu kusimamia gharama ambayo tayari zimeshaonekana.

Kwa maneno mengine Kenya itahitajika kwanza kutumia gharama zake kupeleka askari Haiti kabla haijapewa fedha na Umoja wa Mataifa. Kwa hivyo italazimika Kenya kutafuta nchi itakayokuwa tayari kuipatia fedha moja kwa moja.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW