1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya bingwa CECAFA, Zanzibar mashujaa

Sekione Kitojo
18 Desemba 2017

Harambee Stars  ya  Kenya  yanyakua  kombe  la  Challenge la Cecafa , lakini  gumzo  kubwa  ni  kuhusu  timu  ya  Zanzibar  heroes, yapokewa kwa shangwe kubwa mjini Unguja

CECAFA Fussball-Cup
Michuano ya cecafa, Afrika mashariki na katiPicha: EBRAHIM HAMID/AFP/Getty Images

Kenya  imeshinda  kombe  la  Challenge  la  shirikisho  la  vyama vya  kandanda  Afrika  mashariki  na  kati Cecafa  jana  Jumapili wakati  walipoishinda Zanzibar Heroes  kwa  mabao 3-2  katika mikwaju  ya  penalti  kufuatia  sare  ya  mabao 2-2  hadi  mchezo kumalizika  kwa  dakika  za  nyongeza  mjini  Machakos  nchini Kenya.

Timu ya taifa ya Kenya inayofahamika kama "Harambee stars" imenyakua kombe la Challenge la cecafaPicha: DW

Ovella Ochieng  aliipatia  wenyeji  Kenya  bao  la  kuongoza katika  dakika  ya  tano  ya  mchezo, lakini  Zanzibar  wakiwania ubingwa  wao  wa  kwanza  tangu  miaka  22  iliyopita, ilisawazisha katika  dakika  ya  87  kwa  bao  la  khamis Mussa. Kenya  ilipata bao  tena  la  kuongoza  dakika  saba  katika  kipindi  cha  kwanza cha  nyongeza  wakati  Masood Juma  alipotumia  makosa  ya mlinda  mlango  wa  Zanzibar, lakini  Zanzibar Heroes  walirejesha bao  hilo  kwa bao  tena  la  Mussa na  kusababisha  mchezo  huo kuamuliwa  bkwa  mikwaju  ya  penalti.

Mlinda  mlango  wa  Kenya Patrick Matasi alikuwa  nyota  katika  mikwaju  ya  penalti akiokoa mikwaju  mitatu  na  kuchaguliwa  kuwa  mchezaji  bora  wa mashindano  hayo.

Timu  ya  taifa  ya  Zanzibar Zanzibar Heroes  ilipokelewa  kwa shangwe  kama  mashujaa  wa  kweli  mjini  Zanzibar  leo  mjini  Unguja.

Mwaka 1995  Zanzibar  kwa  mara  ya  kwanza  ilifanikiwa  kunyakua kombe  hilo  lakini  limekuwa  ndoto  tangu  wakati  huo  na mwaka huu  timu  ya  taifa  ya  Zanzibar, Zanzibar Heroes  imeshangaza kila shabiki  wa  kandanda  katika  Afrika  mashariki  na  kati  pale ilipoanza  kwa  kuiangusha  Rwanda  kwa  mabao 3-1 na  kisha kuikandika  Tanzania  bara  kwa  mabao 2-1  na  pia  Uganda mabingwa  watetezi  wa  kombe  hilo  linaloshindaniwa  kila  mwaka kwa  mabao 2-1  pia.

Nilizungumza  na  mchambuzi  wa  masuala  ya kandanda  wa  DW  na  ambaye  hivi  sasa  yuko  Zanzibar  kwa mapumziko  Ramadhan Ali , ambaye  pia  aliwahi  kuichezea  timu hiyo  ya  taifa  Zanzibar  Heroes katika  miaka  ya  60 wakati  wa kombe  la  Gossege. Nilimuuliza  kuhusu  historia  ya  Zanzibar kucharuka   na  mara  kurudi  nyuma  katika  kandanda  la  Afrika mashariki na  kati.

Ni  mara  ya  saba  Kenya  kunyakua  kombe  hilo, mara  hii  kwa uongozi  wa  kocha  mpya  Paul Put  akipata  mafanikio  yake  ya kwanza  tangu  alipoanza  kuifunza  timu  hiyo  ya  taifa  mwezi uliopita. Mabingwa  wa  zamani  Uganda waliishinda  Burundi  kwa mabao 2-1  na  kushika  nafasi  ya  tatu.

Bundesliga

Kwa upande  wa  Bundesliga  ligi  kuu  hapa  Ujerumani , mwishoni mwa  juma  ilitimiza mchezo  wake  wa  17 , na  kwa  kawaida unakuwa  mchezo  wa  mwisho  katika  duru  ya  kwanza   ya  msimu. Bundesliga  inakwenda  mapumziko  hadi  tarehe  12 Januari  2018 ambapo  ligi  hiyo  itarejea  tena  viwanjani  ambapo Leverkusen itakuwa  mwenyeji  wa  FC Bayern Munich.

Wachezaji wa VFB Stuttgart wakipambana na wachezaji wa Bayern MunichPicha: Getty Images/T.Kienzle

Hadi  katika  mchezo  huo  wa  17, Bayern Munich  inaongoza  kwa kuwa  na  pointi 41 , ikiwa  mbele  kwa  pointi  11  kutoka  timu inayoifuata  Schalke  04  ambayo  ina  pointi 30  baada  ya  kutoka sare  ya  mabao  2-2  na  Eintracht  Frankfurt siku ya  Jumamosi. RB Leipzig iliyokuwa  ikishikilia  nafasi  ya  pili imeporomoka  hadi nafasi  ya  5 baada  ya  kukandikwa  mabao 3-2  na  Hertha Berlin jana  Jumapili.

Borussia Dortmund  ambayo  iliachana na  kocha  wake Peter Bosz, na kumpa kazi  hiyo  Peter Stoeger  ilizinduka  katika  michezo  miwili ya  mwisho  na  kupata  ushindi  ambapo iliibuka  na  ushindi  wa mabao  2-1  siku  ya  Jumamosi  dhidi  ya  Hoffenheim. BVB inashika  sasa  nafasi  ya  3  ikiwa  na  pointi 28.

Wachezaji wa Borussia Dortmund wakifurahia baoPicha: Reuters/L. Kügeler

Mabao  manane  yalitinga  nyavuni  jana  Jumapili  katika  pambano kati  ya  Hannover  dhidi  ya  Bayer Leverkusen   ambapo  mchezo huo  ulimalizika  kwa  sare  ya  mabao 4-4  na  Leverkusen  kupoteza fursa  ya  kuchupa  hadi  nafasi  ya  pili  katika  msimamo  wa  ligi  na kubakia  katika  nafasi  ya  nne  ikiwa  na  pointi 28  nyuma  ya Borussia  Dortmund.

Kombe la  DFB

Lakini  kabla  mwaka  haujamalizika  kuna  patashika  nyingine inatarajiwa  siku  ya  Jumatano  wakati  Bayern Munich itakapopambana  na  Borussia  Dortmund  katika  mchezo  wa kufunga  mwaka  wa  kombe  la  shirikisho , DFB Pokal. ushindi mara  mbili  mfululizo  wa  kocha  mpya  Peter Stoeger  umeiamsha Dortmund  katika  mzingizi  mzito  wa  majira  ya  baridi  na inakumbana  na  Bayern Munich siku  ya  Jumatano  ikiwa  na  hali mpya  ya  kujiamini.

Mainz  na  VFB Stuttgart  zitaanza  kuwania  nafsi  ya  kucheza katika  robo  fainali  ya  kombe  la  shirikisho  kesho  Jumanne, ambapo  pia  schalke  04 itakwaana  na FC Kolon  ambayo  ilipata ushindi  wake  wa  kwanza katika  Bundesliga   msimu  huu baada  ya kuiangusha  Wolfsburg  kwa  bao 1-0.

Wachezaji wa Leverkusen Bellarabi na Bailey wakishangiria baoPicha: picture-alliance/dpa/P. Steffen

Nuerenburg  itawakaribisha  VFL Wolfsburg katika  mchezo mwingine  na  Ingolstadt  itakuwa  wageni  wa  Parderborn.

Siku  ya  Jumatano  Bremen  itaumana  na  freiburg  katika  pambano la  timu  za  ligi  daraja  la  kwanza  Bundesliga , Gladbach itaikaribisha  Leverkusen  na  Heidenheim itakuwa  wenyeji  wa Frankfurt.

Katika  ligi  ya  England , Premier League , Kocha Jurgen Klopp anakiri  kwamba  Manchester  City haitakuwa  rahisi  kuikamata , lakini  kocha  huyo  wa  Liverpool  atafurahi  iwapo  ataweza  hata kunyakua  nafasi  moja  kati   ya  nne  za  juu.

Liverpool  iliishinda  Bournemouth  kwa  mabao 4-0  na  kujiweka katika  nafasi  ya  nne , pointi  4  nyuma  ya  Chelsea  iliyoko  katika nafasi  ya  tatu .  Lakini  kocha  wa  Manchester  United  mahasimu wakubwa  wa  Manchester City Jose Mourinho  amesisitiza  kuwa timu  yake  haitakata  tamaa  katika  kinyang'anyiro  cha  kuwania taji  la  ligi  hiyo baada  ya  pointi  za  uongozi  za  Manchester punguzwa  hadi  pointi 11  na  Machester  United  iliyoko  katika nafasi  ya  pili. Kikosi  cha  Jose Mourinho  kiliishinda  West Bromwich  jana  Jumapili  kwa  mabao 2-1.

Kocha wa Manchester United Jose MourinhoPicha: picture-alliance/dpa/M.Rickett

Wakati  huo  huo Manchester City  itafanya  mazungumzo  na  kocha Pep Guardiola mwishoni  mwa  msimu  kuhusu  kuongeza mkataba wake  kwa  miaka  mitatu, vimesema vyombo  vya  habari  vya Uingereza.

Mchezaji  wa  zamani  wa  timu  ya  taifa  ya  Brazil Kaka ametangaza  kwamba  anatundika  madaluga  juu  na  kufikisha mwisho  muda  wake  wa  kucheza soka  ya  kulipwa, jana  akidokeza kwamba  huenda  akaamua kuingia  katika   kazi  ya  uongozi katika kilabu  yake  ya  zamani AC Milan.

Mchezaji wa zamani wa Brazil KakaPicha: picture-alliance/dpa

Mlinda  mlango  Peter Gulacsi  amerefusha  mkataba  wake  na RB Leipzig  ya  Ujerumani  hadi  mwaka  2022, imesema  klabu  hiyo ya  Bundesliga  jana  Jumapili.

Wakati  huo  huo  mshambuliaji  wa  Borussia  Dortmund  raia  wa Gabon  Pierre-Emerick Aubameyang  amerefusha  pia  mkataba wake na  klabu  hiyo  hadi  mwaka  2021 vimeripoti  vyombo  vya  habari vya  Ujerumani  jana Jumapili.

Mwandishi: Sekione  Kitojo / afpe / rtre / dpae

Mhariri: Mohammed Khelef