1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SafariKenya

Maonesho ya utalii Afrika Mashariki yataleta tija?

wakio Mbogo20 Novemba 2023

Maonesho ya Utalii ya Afrika Mashariki, 'East African tourism Expo', yameanza hapo jana mjini Nairobi, Kenya, yakiwaleta pamoja washiriki kutoka mataifa 32 ulimwenguni.

Utalii | Watalii katika matembezi
Watalii katika matembeziPicha: Ishara S. Kodikara/AFP/Getty Images

Maonesho hayo yanalenga kuimarisha utalii katika kanda ya Afrika Mashariki, kukuza uwekezaji katika sekta za hoteli, usafiri wa utalii.

Hata hivyo baadhi ya wadaua wa sekta hiyo wanalalamikia tozo kubwa kwa watalii na hali mbaya kwenye viwanja vya ndege, ambavyo wanasema vinaathiri utalii. 

Maonyesho ya utalii ya kanda ya Africa Mashariki yaliyoanza Jumatatu yanatoa fursa kwa watoa huduma kwenye sekta ya utaliina washirika wa kibiashara kuja pamoja kwa malengo ya kutatua masuala mbalimbali yanayotatiza utalii kwenye kanda nzima ya Afrika Mashariki.

Soma pia:Maonyesho ya utalii ya nchi za Afrika Mashariki mjini Arusha

John Olooltua, katibu mkuu wa wizara ya Utaliij nchini Kenya amesema kwa kuweka juhudi za pamoja za kuuza utalii wa mataifa ya Afrika Mashariki, inakuwa njia ya kulifanya eneo zima kuvutia watalii kutoka kila pembe ya dunia.

"Tunajivunia maonyesho haya na uwezo wa kushirikiana na wadau mbalimbali nchini kuonyesha vivutio na utamaduni wetu.” Alisema.

Maonyesho hayo ya siku tatu yanayofanyika hadi tarehe 22, kwenye ukumbi wa jumba la kimataifa la KICC, Nairobi, yamewajumuisha waonyeshaji 286 kutoka mataifa mbalimbali ulimwenguni.

GIZ: Utalii unachangia uchumi wa Afrika Mashariki

Bjoern Ritcher, mratibu katika shirika la maendeleo la Ujerumani, GIZ, ameusifia utangamano wa mataifa ya Afrika Mashariki kama njia mojawapo ya kuimarisha uchumi kati ya mataifa wanachama.

Zanzibar kisiwa chenye utajiri wa fukwe za kuvutiaPicha: DW

Kati ya miradi inayofanikishwa na shirika la GIZ ni mradi wa ‘Visit East Africa-Feel the Vibe', mradi wa kipekee unaoangaza vivutio vinavyopatikana Afrika Mashariki.

"Utalii unachangia kiwango kikubwa cha uchumi wa mataifa yote saba ya Afrika mashariki,"

Ritcher aliongeza kwamba "pia unachangia zaidi ya asilimia saba ya ajira kwenye ukanda huu. Kwa hiyo utangamano wa mataifa haya una mafanikio makubwa.”

Hata hivyo baadhi ya wadauwanaikosoa wizara ya utalii kwa kuongeza ada ya visa kwa watalii wanaoingia nchini, utozaji ushuru wa bidhaa binafsi zinazopita dola mia tano na hali mbaya ya viwanja vya ndege nchini.

Soma pia:Msumbiji yautangaza upya utalii wake

Mbunge wa Kilifi Kaskazini owen Baya anasema changamoto hizi zinazojitokeza wakati utalii unayumbayumba, huenda zikashusha zaidi idadi ya watalii wanaozuru Kenya.

"Tunawapoteza watalii kwa mataifa mengine kwa sababu ya vikwazo vyetu." Baya aliiambia DW.

Alisema hatua hiyo inasababisha watu kughairi safari zao kuingia nchini kwa sababu ya picha zilizosambazwa mtandaoni zikionesha hali ilivyo kwenye uwanja wa kimataifa wa JKIA.

Hii ni awamu ya tatu ya maeonyesho hayo ya kikanda ya utalii. Awamu ya kwanza ilifanyika nchini Tanzania, na mwenyeji wa pili wa maonyesho hayo lilikuwa taifa la Burundi mwaka uliopita.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW