Kenya, Eritrea zakubaliana kuondoa viza kwa wananchi wao
10 Februari 2023Wakizungumza wakati wa mazingumzo ya mahusiano, marais William Ruto na Isaias Afwerki walielezea kuwa hatua hiyo itachochea ukuaji wa uchumi wa mataifa hayo.
Marais hao wawili waliafikiana kuwa pana uwezo mkubwa wa biashara na uwekezaji kati yao huku wito wa ushirikiano ukitolewa. Eritrea sasa inajiunga na Afrika Kusini ambayo iliwaruhusu Wakenya kuzuru taifa hilo kwa kipindi cha siku 90 bila ya hati ya kusafiria.
Rais Ruto alisema kuwa hatua hiyo iliafikiwa baada ya Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa kuingilia kati.
Wakati huo huo Kenya inapanga kufungua ubalozi wake katika mji mkuu wa Asmara ulioko Eritrea.
Rais Afwerki amekuwa nchini Kenya kwa ziara ya siku mbili, tangu alipowasili siku ya Jumatano.
Mara ya mwisho kwa rais Afwerki kuzuru Kenya kwa ziara rasmi ilikuwa tarehe 15, Desemba mwaka 2018, wakati wa utawala wa rais mstaafu Uhuru Kenyatta.