1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya: Familia yadai jamaa wao aloachiliwa huru amekamatwa

Thelma Mwadzaya9 Oktoba 2020

Mmoja wa waliokuwa watuhumiwa wa shambulio la kigaidi la Westgate, Nairobi, Kenya, Liban Omar, anaripotiwa kukamatwa na watu wasiojulikana muda mfupi baada ya mahakama kumkuta hana hatia.

Liban Abdullah Omar, Mohamed Ahmed Abdi
Picha: Brian Inganga/AP Photo/picture-alliance

Mahakama ilimuachilia huru siku ya Jumatano baada ya kukosa ushahidi wa kumbana kwa kuhusika na shambulio la Westgate la mwaka 2013. Wenzake wawili bado wana kesi ya kujibu na adhabu yao itatangazwa baadaye mwezi huu.

Masaa machache baada ya mahakama ya Milimani kumuachia huru Liban Omar kwa kukosa ushahidi wa kuhusika na shambulio la jumba la biashara la Westgate la miaka 7 iliyopita, familia yake sasa inasema hawajui aliko.

Soma pia:Watuhumiwa wawili wa Westgate wakutwa na hatia, mmoja aachiwa

Duru za polisi zinaeleza kuwa Liban Omar alikamatwa na watu wasiojulikana alipokuwa anaondoka kwenye makao makuu ya kitengo maalum cha kupambana na ugaidi nchini Kenya, ATPU, kilichoko mtaani Upperhill hapa jijini Nairobi.

Liban Omar ni ndugu wa mmoja wa watuhumiwa 4 wa ugaidi waliohusika kwenye shambulio la Westgate mwaka 2013. Kulingana na wakili Mbugua Mureithi, mteja wake Liban Omar alikamatwa mwendo wa saa tano asubuhi hapo jana Alhamisi.

Washukiwa waliokabiliwa na kesi ya kushirikiana na waliofanya shambulizi dhidi ya jengo la kibiashara Kenya Westgate (2013) wakiwa kizimbani Oktoba 5, 2020.Picha: Brian Inganga/AP Photo/picture-alliance

Omar na jamaa zake wanaripotiwa kuwa walikuwa kwenye usafiri wa teksi wakielekea mtaa wa Eastleigh pale watu waliojihami kwa silaha na kufinika nyuso zao walipowavamia na kulisimamisha gari lao.

Kulingana na jamaa zake, watu hao walimkamata Liban Omar na kumlazimisha kuingia kwenye gari aina ya Subaru.

Ili kuhakikisha kuwa wanashindwa kuondoka au kuwafuata, watu hao wasiojulikana kadhalika walichukua funguo za teksi iliyokuwa inawasafirisha Omar na nduguze.

Baada ya muda familia yake ilipiga ripoti kwenye kituo cha polisi cha Capital Hill mwendo wa saa saba mchana. Kufikia sasa, kitengo maalum cha polisi wa kupambana na ugaidi, ATPU, kimekanusha kuhusika na tukio hilo.

Ifahamike kuwa kulingana na utaratibu, watuhumiwa wa ugaidi wanalazimika kupata ridhaa ya kituo au jela aliyokuwa anazuiliwa na kitengo cha kupambana na ugaidi ATPU kabla ya kurejea katika maisha ya kawaida.

Liban Omar alikuwa anazuiliwa kwenye jela ya ulinzi mkali ya Kamiti kabla ya mahakama kumuachilia huru. Kwa kuwa yeye ni raia wa Somalia na mkimbizi, mahakama iliamuru apewe kadi yake maalum ya utambulisho kabla ya kumkabidhisha kwa Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR.

Liban Omar ni mtuhumiwa wa pili kuachiliwa na mahakama baada ya mwenzake, Dheq, kuwa huru mwaka 2019. Washukiwa wenzake wawili waliosalia ambao mahakama imewepata kuwa na kesi ya kujibu watahukumiwa tarehe 22 mwezi huu wa Oktoba.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW