1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mvua yaathiri kaya elfu 80 kote nchini Kenya

21 Novemba 2023

Takriban kaya 80,000 zimeathirika kutokana na mvua ya El nino inayonyesha nchini Kenya wakati idadi ya kaunti zilizoathirika ikiongezeka hadi 33.

Kenia Mombasa 2023 | Überschwemmungen
Abiria wa basi wakiwa katika jitihada ya kujinusuru baada ya basi lao kujaa maji.Picha: REUTERS

Mojawapo ya sehemu zilizoathirika zaidi na mafuriko jimboni Kisumu ni eneo la Nyando ambapo kaya zaidi ya 500 zimelazimika kutafuta hifadhi maeneo salama yenye miinuko huku vijiji vya Ombaka, Kaloo, Kasiwindi Kusini, Kanyipula na Tura vikifurika maji baada ya mto Nyando kuvunja kingo zake.

Kando na waathiriwa wa Nyando kulalamikia kutopokea msaada wowote tangu walipohamishiwa sehemu salama wiki 2 zilizopita, huko Pwani ya Kenya jijini Mombasa, Gavana wa jimbo hilo Abdull Swamad Sharif Nassir anasema serikali yake haijapokea mgao wowote wa pesa kutoka serikali ya kitaifa kupambana na janga la mvua ya El Nino huku takriban watu 3,800 wakiripotiwa kuathirika Mombasa.

Miili ya watu watatu yaopolewa mtoni

Wakazi wa Mombasa wakiwa katika juhudi za kuvushana baada ya barabara zao kujaa maji.Picha: REUTERS

Maeneo mengine yaliyoathirika ni pamoja na Kwale ambapo miili ya watu watatu iliopolewa katika mto Ramisi baada ya kusombwa na mafuriko, huko Turkana miundo msingi ya barabara inayovuka kuelekea Lodwar ikiharibiwa na mafuriko ya maji, Tana River, Wajir.

Shirika la utabiri wa hali ya hewa limeonya kuwa, maeneo ya Kaskazini na Pwani ya Kenya yatapokea mvua nyingi zaidi ikiifuatiwa na Nairobi na eneo la Kati huku takwimu za shirika la Msalaba Mwekundu Red Cross likisajili vifo vya watu 61 kote nchini. Wengine 235 wamejeruhiwa na 8 hawajulikani walipo.

Soma zaidi:Mafuriko yaua watu 14 Kenya, familia elfu 15 zaathirika

Takwimu za shirika la Msalaba Mwekundu za tangu mwezi Oktoba mwaka huu zimesajili uharibifu wa biashara 1,143 , shule 10 na Mifugo 11,610 imeangamia.

Chanzo: DW Kenya

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW