1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya: Idadi ya majaji wanawake yaongezeka

Thelma Mwadzaya 28 Oktoba 2022

Jaji Mkuu wa Kenya Martha Koome amesifu ongezeko la idadi ya majaji wanawake katika mahakama za nchi hiyo akisema ni ishara ya mabadiliko ya mtazamo yanayowapa nafasi wanawake katika fani zote.

Kenia Nairobi Staatshaus Amtseid
Picha: PPS-presidential press service

Akizungumza kwenye kongamano la 17 la majaji wanawake wa kiafrika, Jaji Mkuu Martha Koome, ameipongeza hatua ya kuongeza idadi ya wanawake katika fani ya sheria. Maendeleo hayo yanaakisi mageuzi ya ya mtazamo yanayompa mwanamke nafasi kukwea kwenye nyadhifa  uongozini.

Mbali ya urari wa idadi ya majaji wanawake na wanaume kukaribiana nchini Kenya, idadi ya mawakili wanawake pia imeongezeka. Hivi sasa Kenya  ina mawakili wanawake 295 na ya wanaume ni 298. Ifahamike kuwa jaji mwanamke wa kwanza nchini Kenya alipatikana mwaka 1982.Kwa sasa, idara ya mahakama inaongozwa na jaji mkuu mwanamke,naibu wake na msajili wote ni wanawake.

Majaji wanawake wakiwa ni miongoni mwa majaji wa mahakama kuuPicha: Baz Ratner/REUTERS

Kwenye kongamano la majaji wanawake barani Afrika, wasomi wameshinikiza serikali za kanda kuhakikisha elimu bila malipo inatolewa ili wasichana wengi zaidi waipate pasina vikwazo. Chama cha majaji wanawake barani Afrika,IAWJ,kinawakilisha idara za mahakama kote ulimwenguni lengo likiwa kuimarisha haki na usawa ndani ya sheria.

Ifahamike kuwa Effie Owuor ndiye mwanamke wa kwanza kuwa jaji kwenye mahakama kuu na aliteuliwa mwaka 1982. Mwaka 1998 alijiunga na mahakama ya rufaa na kuwa mwanamke wa kwanza kuhudumu kwenye korti hiyo ya juu.Mwanamke mwengine wa kwanza kuteuliwa kwenye wadhifa huo ni jaji Joyce Aluoch.Majaji Joyce Aluoch na Effie Owuor ndio waasisi wa chama cha majaji wanawake wa Kenya,KWJA, kilichozinduliwa mwaka 1993.Mwito wa Raîla kwa Kenyatta kuhusu uteuzi wa majaji

Wanachama wengine wa mwanzo wa chama hicho ni majaji Roselyn Nambuye,Mary Ang'awa na Sarah Ondeyo waliokuwa mstari wa mbele kuwashajiisha wanawake wengine kujiunga na idara ya mahakama.Joy Mdivo ni wakili wa masuala ya familia ambaye amewahi kuhudumu kama hakimu na huu ndio mtazamo wake.

Kongamano la 17 la majaji wanawake wa Afrika linahitimishwa jumamosi.Kauli mbiu ni majaji wanawake: kuondoa vikwazo vya kutimiza haki na usawa, kuimarisha taasisi.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW