1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya imeishinda Djibouti kiti cha Baraza la Usalama

Yusra Buwayhid
19 Juni 2020

Nchi wanachama 193 wa Umoja wa Mataifa, Alhamisi zimeichagua Kenya kuchukua kiti kinacholiwakilisha bara la Afrika katika Baraza la Usalama la umoja huo, baada ya kuishinda Djibouti katika duru ya pili ya kura.

Mitglieder des Sicherheitsrates der Vereinten Nationen halten zu Beginn einer Sitzung über Afghanistan im Hauptquartier der Vereinten Nationen im Stadtbezirk Manhattan in New York City eine Schweigeminute ein
Picha: Reuters

Mexico, India, Ireland, Norway - waliochaguliwa siku ya Jumatano - pamoja na Kenya iliyochaguliwa jana wataanza rasmi muhula wao wa miaka miwili ijayo katika Baraza hilo lenye wajumbe 15 mnamo Januari 1, 2021. Mexico na India zilichaguliwa bila pingamizi, wakati Ireland na Norway zilichaguliwa baada ya kuishinda Canada.

Kenya, mojawapo ya mataifa yenye nguvu barani Afrika, ilishinda kura 129, na Djibouti, taifa dogo barani humo ilipata kura 62, kama alivyotangaza rasmi Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Tijjani Muhammad-Bande.

"Baada ya kupata idadi kubwa ya kura, Kenya inachaguliwa kuwa mjumbe wa Baraza la Usalama kwa muhula wa miaka miwili utakaoanza Januari 1, 2021. Ninaipongeza Kenya kwa kuchaguliwa kama mjumbe wa Baraza la Usalama," Muhammad-Bande.

Ushindi katika duru ya pili

Ili kuhakikisha uwakilishi wa kijiografia, viti vimetengwa kwa ajili ya makundi tofauti ya kikanda. Katika duru ya kwanza, Kenya na Djibouti zote mbili zilishindwa kupata wingi wa kura, kunyakuwa kiti hicho.

Soma zaidi: Kenya, Djibouti kurudia kura kuwania nafasi ya baraza la UN

Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Tijjani Muhammad-BandePicha: picture-alliance/KEYSTONE/S. Di Nolfi

Baada ya kufanya kazi kupitia njia za kiteknolojia tangu mwezi Machi, kutokana na janga la maambukizi ya virusi vya korona, wanadiplomasia waliokuwa wamevaa barakoa na kuweka umbali unaolazimika kutoka mtu mmoja hadi mwingine, walirudi katika ukumbi wa mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Jumatano na Alhamisi kupiga kura hiyo ya siri katika wakati waliopangiwa.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ni chombo pekee, kinachoweza kufanya maamuzi ya kisheria kama vile kuweka vikwazo na kuidhinisha utumiaji wa vikosi vya wanajeshi. Baraza hilo lina wanachama watano wa kudumu wenye uwezo wa kutumia kura ya turufu ambao ni Marekani, Uingereza, Ufaransa, China na Urusi. Na kila mwaka, zinachaguliwa nchi tano tofauti za kujaza viti kumi vya wanachama wasio wa kudumu.

Vyanzo: (dpa, rtr, rtrtv)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW