1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya yakabiliwa na duru mpya ya maandamano

19 Julai 2023

Kenya inakabiliwa leo na duru mpya ya maandamano licha ya serikali kuonya kwamba haitavumilia machafuko zaidi baada ya maandamano ya awali kusababisha vifo vya watu zaidi ya 10.

Waandamanaji waandamana katika mtaa wa Lang'ata jijini Nairobi mnamo Mei 2, 2023
Maandamano jijini Nairobi nchini KenyaPicha: John Ochieng/SOPA/ZUMA/IMAGO

Maeneo kadhaa ya nchi yakiwemo mitaa mbalimbali ya Nairobi na Kisumu kwa sasa yanashudia makabiliano kati ya waandamanaji na polisi. Polisi wanawafyatulia mabomu ya kutoa machozi waandamanaji wanaoonekana kuwasha moto matairi barabarani.

Upinyani umeapa kufanya maandamano kwa siku tatu

Upinzani umeapa kufanya maandamano kwa siku tatu mfululizo dhidi ya serikali ya Rais William Ruto, na kusababisha jumuiya ya kimataifa kujiunga katika kutoa wito wa kupatikana suluhisho la kisiasa katika mzozo huo. Shule za kutwa na maduka yamefungwa katika mji mkuu wa Nairobi na miji mingine, huku waandamanaji wakihimizwa kubeba sufuria na kuingia mitaani. Kulingana na afisa wa polisi aliyezungumza kwa sharti la kutotambulishwa, waandamanaji wanne walijeruhiwa katika eneo la Mathare jijini Nairobi.

Viongozi wa kidini watoa wito wa mazungumzo

Kiongozi rasmi wa upinzani nchini Kenya - Raila OdingaPicha: James Wakibia/Zuma/picture alliance

Viongozi wa kidini wamekuwa wakitoa wito wa mazungumzo kati ya viongozi wa serikali na upinzani kusitisha maandamano hayo. Maaskofu wa kanisa katoliki wakiongozwa na  Anthony Muheria. leo walitoa taarifa inayosisitiza kuwa hakuna umwagikaji damu zaidi unaopaswa kuendelea na kumuhimiza rais kufuta sheria mpya ya fedha iliyopitishwa na kuwaghadhabisha wananchi. Haki ya maandamano ya amani imetaribishwa katika katiba ya Kenya lakini upinzani katika siku za nyuma umefanya maandamano ya ghasia yaliosababisha vifo.

Viongozi wa nje pia watoa wito wa kusitishwa kwa maandamano

Wajumbe wa Magharibi kutoka mataifa 13 hapo jana walitoa taarifa ya pamoja ya mazungumzo na kuelezea wasiwasi wao kuhusu kupotezwa kwa maisha na kuharibiwa kwa mali. Shirika la kutetea haki la Human Rights Watch, limewahimiza viongozi wa kisiasa kukoma kuwataja waandamanaji kuwa magaidi na kuheshimu haki yao ya maandamano ya amani. Shirika hilo limetoa wito kwa polisi kukoma kutumia nguvu na risasi za moto kukabiliana na waandamanaji.

Hii ni mara ya tatu ndani ya mwezi huu kwa kiongozi wa upinzani Raila Odinga kuandaa maandamano makubwa dhidi ya serikali anayosema si halali na inahusika na mgogoro wa kupanda gharama ya maisha.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW